Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anawakera mapemaaa!

SIMBA na Azam wana jambo lao jioni ya leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati timu hizo zitakapokuwa zikila kiporo chao cha Ligi Kuu Bara msimu huu, huku mashabiki wa timu zotre wakiwa na kiu ya kuona nyota wao wakiwakera wenzao.

Huko Msimbazi kwa sasa gumzo kubwa ni kurejea kwa kasi kwa Bernard Morrison, huku Larry Bwalya naye akiwa yupo moto kinoma, bila kuwasahau kina Luis Miquissone na Meddie Kagere ambaye msimu uliopita aliwalaza njaa Azam mara mbili kwa kufunga mabao ya ushindi.

Kagere alifunga bao pekee lililoizamisha Azam katika mechi ya mkondo wa kwanza wa ligi msimu huo iliyopigwa Oktioba 23, kisha kufunga bao la tatu katika ushindi wa Simba wa 3-2 dhidi ya wauza lambalamba hao waliporudiana tena Machi 4 Azam wakiwa wenyeji.

Mabao mengine kwenye mchezo huo yalifungwa na Erasto Nyoni aliyesawazisha bao la mapema la Azam lililowekwa kimiani na Never Tigere na Deo Kanda anafunga la pili kabla na kipindi cha Idd Seleman ‘Nado’ akasawazisha ndiko Kagere akamaliza udhia kwa kupiga bao la tatu na la ushindi.

Hivyo, mchezo wa leo ambao ni kati ya mechi mbili za viporo zinazochezwa likianza kiporo cha Namungo FC dhidi ya Ruvu Shooting mapema jioni kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi kisha ndipo usiku mechi ya kisasi itapigwa kwa Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Wageni Azam wanaingia katika mechi hiyo wakiwa na hamu ya kulipa kisasi cha unyonge wa misimu mitano mfululizo mbele ya Simba katika mechi za Ligi Kuu ambapo imepoteza idadi kubwa ya mechi pindi inapokutana na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.

Katika misimu mitano iliyopita, timu hizo zimekutana mara 10 katika Ligi Kuu ambapo Simba imeibuka na ushindi mara tano, zikitoka sare mara nne huku Azam FC ikiibuka na ushindi mara moja tu.

Lakini ukiondoa hilo, mchezo wa leo ni muhimu kwa kila timu kujiweka katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa kulingana na msimamo wa Ligi Kuu msimu huu ulivyo.

Wenyeji Simba walio na pointi 38, wanahitaji ushindi ili kupunguza pengo la pointi baina yake na Yanga kubakia pointi tatu huku pia wakibakiwa na mechi moja ya kiporo ambayo kama watashinda, watakwea kileleni mwa msimamo wa ligi lakini kama watapoteza maana yake watawafanya Yanga wawe na uhakika wa kubakia kileleni mwa msimamo wa ligi hata kama watakuja kushinda mechi yao moja ya kiporo itakayobakia baada ya mechi ya leo.

Kwa Azam walio katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi, ushindi leo utawafanya wafikishe pointi 35 na kupunguza pengo baina yao na vinara kufikia tisa lakini kama watapoteza, maana yake watazidiwa na Yanga kwa pointi 12 huku Simba ikiwaacha kwa pointi tisa, jambo ambalo ni wazi kwamba litafifisha matumaini yao ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Ni mechi ambayo Simba itaingia ikiitegemea zaidi safu yake ya kiungo inayoundwa na Taddeo Lwanga, Bwalya, Luis, Morrison na fundi wa mpira Clatous Chama ambayo ndio imekuwa mhimili wa kuifanya timu hiyo imiliki mpira, kutengeneza nafasi na kufunga mabao.

Morrison amerejea na makali mapya kwani katika mechi tatu akiwa chini ya Kocha Gomes, amefunga mabao matatu na kuasisti mawili, huku akionekana kuwakera Yanga ambao hawana furaha naye tangu alipowahama kihuni kutua kwa watani wao.

Kwa upande wa Azam, yenyewe inawategemea zaidi washambuliaji wake, Obrey Chirwa, Mpiana Mozinzi, Prince Dube na Idd Selemani ‘Nado’ kupeleka madhara langoni mwa Simba kutokana na makali yao ya kufumania nyavu.

Wakati Simba wakiingia wakiwa kamili katika mechi ya leo, Azam yenyewe itawakosa wachezaji watatu kutokana na sababu mbalimbali ambapo Yakubu Mohamed atakosekana kwa sababu ya kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano, Frank Domayo na Abdul Hamahama walio majeruhi.

Kocha wa Simba, Didier Gomez alisema wanalazimika kushinda mechi hiyo ili wajiweke sawa kwa kisaikolojia kwa ratiba ngumu iliyo mbele yao ya ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa.

“Ni jambo la muhimu kuhakikisha tunashinda ili tupunguze pengo la pointi baina yetu na Yanga. Tumejipanga vyema kuhakikisha tunashinda kwa sababu ratiba sio rahisi, kwani baada ya hapo tutakabiliana na AS Vita ugenini kisha tutakuwa na mechi dhidi ya Yanga na Al Ahly hivyo tunatakiwa kukusanya pointi kadri iwezekanavyo,” alisema Gomez.

Kocha msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati alisema kuwa timu yake iko tayari kwa mchezo huo na hawatishwi na ubora wa Simba.

“Timu iko vizuri kwa kila kitu tumejaribu kukiweka vizuri. Tunaimani kwamba kesho wachezaji watatupa kila walichonacho kwa jinsi tulivyojitayarisha. Nina imani mambo yatakuwa mazuri.

Kwenye soka kuna mambo mawili. Ukiwa na mpira lazima ushambulie,” alisema Vivier na kuongeza;

“Sisi tumejiandaa kushambulia na tukipoteza mpira ni jukumu la kila mchezaji kukaba. Hatuwezi kubaki nyuma. Ni lazima tukabe juu ili tuweze kupata matokeo mazuri. Simba ni timu nzuri. Wanashiriki mashindano ya kimataifa. sasa kuna kuwa vizuri na kuna matatizo wanayo.”

“Sasa yale matatizo waliyonayo sisi tumeyafanyia kazi. Nina imani kwanza tutawanyima nafasi ya kucheza. Tuwe na mpira kwa muda mrefu tutakuwa tumefaulu, tutakamilisha mpango wetu. Wachezaji wote wako vizuri na wako tayari kupambana,” alisema Bahati.


LINDI NAKO

Mkoani Lindi nako kuna kazi wakati wenyeji Namungo wataikaribisha Ruvu Shooting ambao msimu huu wameonekana kuwa moto na makocha wa timu zote wametamba kwamba hautakuwa mchezo mwepesi.

Namungo inaikaribisha Ruvu ikitoka kuchachiwa na kiporo chao mbele ya KMC kwa kubugizwa mabao 3-0 na ikipambana kujinasua kutoka kwenye eneo la mstari mwekundu wa kushuka daraja.

Kocha Hemed Morocco alisema wameshasoma makosa yao yaliyowaponza kwa KMC na leo watakuwa na kazi moja ya kuwanyoosha Wazee wa Kupapasa inayonolewa na Charles Boniface Mkwasa aliyekiri mchezo wa leo ni mgumu, lakini ni lazima wapambane wapate pointi tatu muhimu.

Ruvu ipo nafasi ya nne ikiwa na alama 28 kutokana na mechi 17 na kaka itashinda itazidi kujichimbia mizizi kwenye nafasi hiyo kwa kufikisha pointi 31, moja pungufu na walizonazo Azam ilipo juu yao.

Ushindi wowote utaivusha Namungo kutoka nafasi ya 15 hadi ya 12 ikizishusha JKT Tanzania na Coastal Union zenye pointi 20 kila moja kwa sasa, kwani wenyewe itafikisha alama 21.