Ally Champion ashinda uongozi ATPBRO
Muktasari:
- Uchaguzi huo mdogo ulisimamiwa na mwenyekiti, wakili Danstan Nyakamo na wajumbe wa kamati, Imani Makongoro na Donald Madono ulipewa baraka na Rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
BONDIA mkongwe, Ally Bakari Champion amechaguliwa kuwa mjumbe wa Chama cha waamuzi wa Ngumi za Kulipwa Tanzania (ATPBRO) katika uchaguzi mdogo uliofanyika leo Aprili 15, jijini Dar es Salaam.
Champion amepata kura 17 huku mpinzani wake, Mwinyimkuu Rajabu akipata kura 9.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa alitaka makundi ya uchaguzi yavunjike.
"Uchaguzi umeisha, sasa makundi yavunjike turudi kwenye utaalamu, mwende kusimamia haki kwenye mapambano, na TPBRC hatutamfumbia macho mwamuzi atakayekwenda kinyume.
"Nilipoingia TPBRC nilikuta waamuzi wanapangwa na Kamisheni, nikasema hapana, mamlaka hayo yanerudishwa kwenye chama chenu, hivyo msilete urafiki katika kutoa matokeo, kwani watu pia wanaona, ngumi zinachezwa hadharani," amesema Palasa aliyeambatana na kaimu katibu mkuu wa TPBRC,Elias Mlundwa.
Mwenyekiti wa uchaguzi, wakili Danstan Nyakamo aliwapongeza wapigara kwa utulivu na kushiriki katika mchakato huo huku katibu mkuu wa ATPBRO, Emmanuel Mlundwa akisisitiza safu ya uongozi kukamilika.
"Tutakwenda vizuri kwenye upangaji wa waamuzi ili kusiwepo na malalamiko, hivi karibuni kuna mapambano Tanga, Morogoro na Dodoma, hivyo upangaji wa waamuzi utazingatiwa," amesema.
Champion aliwashukuru wapigakura kwa kumchagua akisisitiza wote ni wamoja ndani ya Chama hicho na wakisikilizana na kuelekezana watafikia malengo.