Al Ahly yaitibulia Simba Kwa Mkapa

SIMBA ina dakika 90 za kutimiza ndoto za kurudia rekodi ya kufika nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Al Ahly ya Misri katika mechi ya marudiano ya robo fainali baada ya jana usiku kufungwa bao 1-0 na kutibuliwa rekodi yao ya Kwa Mkapa mbele ya watetezi hao wa taji.

Simba ilikumbana na kipigo hicho cha kwanza nyumbani mbele ya Al Ahly katika michuano ya CAF tangu mwaka 1985 baada ya kosa lililofanywa na ukuta wa timu hiyo na kuwapa wageni bao la mapema la dakika ya nne tu ya mchezo lililowakata stimu mashabiki waliojitokeza kwenye Uwanja wa Mkapa.

Bao la Al Ahly yenye rekodi ya kucheza fainali nne mfululizo katika misimu mitano iliyopita na kutwaa taji mara tatu, liliwekwa kimiani na Ahmed Koka baada ya mpira uliokolewa na kipa Ayoub Lakred kumkuta katika nafasi nzuri na kutupia nyavuni.

Bao hilo lilitokana na shambulizi la kushtukiza kupitia pembeni na nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kulambwa chenga na Percy Tau aliyepiga krosi iliyokolewa vibaya na Henock Inonga na kuonekana unaenda nyavuni, lakini Ayoub akauokoa na mfungaji kupigilia msumari.

Huo ni ushindi wa kwanza kwa Al Ahly mbele ya Simba katika mechi tisa walizokutana katika michuano ya CAF tangu mwaka 1985, lakini bado Simba ina nafasi ya kupindua meza katika mechi ya marudiano itakayopigwa jijini Cairo, Ijumaa ijayo itakayoamua timu ya kwenda nusu fainali ya michuano hiyo.


KILICHOWAPONZA

Hata hivyo, mechi hiyo ya marudiano ni kibarua kigumu kwa Simba iwapo itacheza kama ilivyocheza jana na washambuliaji wa timu hiyo walipoteza nafasi nyingi za wazi na mipira mbele ya nyota wa Al Ahly, licha ya kutawala sehemu kubwa ya pambano hilo lililochezeshwa na mwamuzi Abongile Tom kutoka Afrika Kusini.

Katika mchezo wa jana, Kocha Abdelhak Benchikha alimwanzisha Kibu Denis, aliyeisumbua ngome ya Al Ahly, huku Sadio Kanoute alicheza kama mshambuliaji, lakini hakuwa katika ubora kabla ya kutolewa kipindi cha pili.

Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Kibu aliyekuwa na mchezo mzuri walipoteza nafasi nyingi kipindi cha kwanza na hata cha pili, huku Al Ahly ikitumia uzoefu na kucheza kwa umakini kulinda bao hilo lililowasogeza kwenye mlango wa kuingia nusu fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa.


MCHEZO ULIVYOKUA

Timu zote zilianza pambano kwa kasi na kusomana, lakini iliichukua dakika nne tu Al Ahly kupata bao hilo pekee na kumtibulia Kocha Benchikha aliyeifunga Al Ahly katika mechi ya CAF Super Cup mwaka jana wakati akiwa na USM Alger ya Algeria.

Pamoja na Simba kufanya jitihada za kutaka kurudisha bao hilo lakini mastaa wake baadhi walikosa umakini eneo la mwisho na kufanya dakika 45 za kwanza kumalizika ikiwa nyuma kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko akitoka Kanoute na kuingia Willy Onana aliyeongeza nguvu eneo la ushambuliaji kabla ya kuwaongeza tena baadae Pa Jobe na Mzamiru Yasin waliochukua nafasi ya Saido na Sarr.

Baadae aliwaongeza tena Luis Miquissone aliyechukua nafasi ya Kibu na  Israel Mwenda kuchukua nafasi ya Shomary Kapombe.

Licha ya Simba kucheza kwa utulivu hasa katika eneo la kiungo na mabeki wakiidhibiti Al Ahly hususan washambuliaji wao Percy Tau na Modeste waliotolewa kipindi cha pili, lakini bado wageni walionekana tishio na dakika za lala salama baada ya kufanya mabadiliko, iliamua kupaki basi kulinda ushindi huo.

Simba inayotarajiwa kuondoka Jumanne ijayo itakuwa na kazi ya kutumia dakika 90 za mechi ya marudiano ugenini ili kuweka rekodi iliyowahi kuweka mwaka 1974 ilipovaana na Mehalla El Kubra pia ya Misri iliyoing’oa kwa penalti 3-0 baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1 kila timu ikishinda nyumbani kwa bao 1-0.

Lakini 1979 Simba iliwahi kufungwa na Mufurila Wanderers ya Zambia kwa mabao 4-0 nyumbani katika michuano hiyo ya CAF na kwenda kupindua meza ugenini kwa kuifumua 5-0 na kuwaduwaza Wazambia kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-4 rekodi ambayo imeendela kudumu hadi leo.


Vikosi vya jana;

Simba: Ayoub, Kapombe/Mwenda, Tshabalala, Che Malone, Inonga, Sarr/Mzamiru, Kibu/Luis, Ngoma, Kanoute/Onana, Chama na Saido/Pa Jobe

Al Ahly: Shobeir, Almonem, Rabia, Hany, Maaloul, Ateya/Afsha, Koka, El Soulia, El Shehat/Slim, Tau/Taher na Modeste/Kahraba