AKILI ZA KIJIWENI: Tabora ishini kipato chenu

Muktasari:

  • Kama unapata kipato kidogo hakuna sababu ya kulazimisha kuishi maisha ya kipato kikubwa kwani athari zake huwa kubwa kuliko faida unazoweza kuzipata kama ukiamua kufanya hilo.

MIONGONI mwa kanuni kuu za maisha ambazo zinaweza kumfanya mtu aepuke mengi ni mwanadamu kuishi kulingana na kipato chake.

Kama unapata kipato kidogo hakuna sababu ya kulazimisha kuishi maisha ya kipato kikubwa kwani athari zake huwa kubwa kuliko faida unazoweza kuzipata kama ukiamua kufanya hilo.


Kulazimisha kuishi nje ya kipato chako ni mateso na unakaribisha kudhalilika kwa vile kuna wakati utakwama na kila mmoja ataliona hilo na mifano iko mingi kwenye dunia hii kuanzia miaka mingi iliyopita.


Nimeziona taarifa kwenye kitandao ya kijamii zikihusisha timu ya Tabora United nikakumbuka hili la kuishi kulingana na kile unachokipata kwani kuna uhusiano mkubwa na kinachotokea.


Kuna taarifa za changamoto ya kiusafiri ambayo imekikuta kikosi cha vijana cha Tabora baada ya moja kati ya tairi la basi lililowabeba wachezaji wa timu hiyo kwenda Geita ambako walikuwa na mechi ya ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kuharibika na hakukuwa na uwezekano wa kununuliwa kwa tairi jipya ambalo lingefanya kikosi kisafiri vizuri pasipo changamoto yoyote.


Nilivyoziona taarifa hizo nikakumbuka Tabora United imejaza wachezaji kibao wa kigeni kwenye kikosi chake ambao inalazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwahudumia huku timu ikiwa haipo kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.


Nikakumbuka baada ya kuachana na kocha wake Goran Kopunovic, timu hiyo imechukua makocha wawili wa kigeni ambao ni mkuu na msaidizi wake na gharama zao sio za mchezo huku ligi ikiwa imebakisha raundi chache tu kumalizika.


Baada ya hapo nikajiuliza inawezekana vipi klabu ambayo inaweza kutumia fedha nyingi kusajili wachezaji wa kigeni na kuchukua makocha wa kigeni ikakosa fedha kiasi cha kawaida tu kununua tairi la basi ili kikosi chake cha vijana kiweze kusafiri vizuri?


Kuna namna Tabora United inapaswa kujitazama katika upande wa matumizi yake ili iepuke mambo kama haya kwani hayaiweki taswira ya klabu vizuri.