Ajenda ya uchaguzi yawagonganisha wajumbe Riadha Taifa

Ajenda ya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya makamu wa rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na mjumbe mwakilishi wa kanda ya Pwani imeibua mvutano wa wajumbe kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho hilo.

RT inafanya uchaguzi mdogo na mkutano mkuu leo Novemba 27 mjini Dodoma baada ya John Bayo na Robert Kalyahe kujiuzulu.

Awali mkutano huo ulipangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Magereza, Msalato mjini Dodoma, ambako dakika chache kabla ya kuanza, saa 4:20 ilitoka oda iliyoelezwa kutoka ya mkuu wa jeshi hatakiwi kuonekana mtu ndani ya ukumbi huo  na wote kutakiwa kutoka nje haraka bila kueleza sababu.

Wajumbe walihamia kwenye hoteli ya African Dream na saa 7:58 mkutano mkuu ulianza.

Baada ya kufunguliwa na mgeni rasmi saa 8:15, rais wa RT, Silas Isangi alisema ajenda inayofuata ni ya uchaguzi mdogo ili watakaochaguliwa kuchukua nafasi zao na kuendelea na mkutano mkuu.

Baada ya kauli hiyo, wajumbe watano walinyoosha mkono, kabla ya mwenyekiti wa riadha Arusha, Gerald Babu kuhoji sababu za kufanya uchaguzi kabla ya mkutano mkuu.

Katibu wake, Rogart Akhwari alikazia akieleza katiba inamtambua rais kama mwenyekiti wa mkutano mkuu, na kumtaka Isangi arudi meza kuu ili kujibu maswali yao na kamati ya uchaguzi itoke meza kuu.

Rais na wajumbe wengine walirejea meza kuu na kujibu hoja, huku msajili akitoa ufafanuzi wa majukumu ya rais na kamati ya uchaguzi, akishauri uchaguzi mdogo kuendelea.

Mvutano uliendelea kwa muda wajumbe wa Arusha wakidai hilo ni kinyume cha katiba, hata hivyo Isangi alitaka utulivu na uchaguzi mdogo ukaendelea, baada ya ajenda hiyo wajumbe watarudi kwenye mkutano mkuu.

Wagombea wa nafasi ya makamu kwenye uchaguzi mdogo ni Shaban Hiki, William Kalaghe na Juma Ikangaa wakati nafasi ya mjumbe mwakilishi wa kanda ya Pwani ni Felix Chunga pekee atakayepigiwa kura ya ndio au hapana.

Kwenye usaili, wagombea wanane, ikiwamo watano wa nafasi ya makamu wa rais walienguliwa.