Mkutano mkuu, uchaguzi mdogo RT mguu ndani mguu nje

Baada yakutimuliwa kwenye ukumbi wa Magereza, Msalato mjini Dodoma, wajumbe wa Mkutano mkuu Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) wako mguu ndani mguu nje kuendelea na mkutano na uchaguzi mdogo.

Ratiba ya RT ilionyesha mkutano kuanza saa 4 asubuhi, lakini ilipofika saa 4:20, mwenyeji wao ambaye hakujulikana mara moja jina lake alitangaza kwamba oda imetoka kwa mkuu wa jeshi, hataki kumuona mtu ndani ya ukumbi huo.

"Hii ni oda, hatakiwi mtu hapa, wote mtoke hadi nje ya geti mara moja," alisema mtu huyo kupitia kipaza sauti na kuondoka ukumbini hapo.

Baada ya tangazo hilo, wajumbe walitoka nje ya geti na kusimama vikundi vikundi kabla ya watu wa Serikali kufika nje ta geti hilo na kuzungumza na uongozi wa RT wakihoji sababu za kutimuliwa.

Wakati rais wa RT, Silas Isangi akieleza kwa msajili, Kaimu katibu mkuu wa RT, Jackson Ndaweka alisogea na kudai kuna kitu kimefanyika japo hataki kukieleza kwa kuwa si rasmi.

Alisema wao RT walilipia na kuruhusiwa kutumia ukumbi huo.

Hata hivyo, rais wa RT aliwataka wajumbe kuelekea kwenye hoteli ya African Dream kwa ajili ya kufanya taratibu zingine.

"Hatujafahamu kama tutafanya mkutano na uchaguzi, tupeni muda tuone kinachoendelea," amesema.

Tangu kufanyika kwa usaili wa wagombea kumekuwa na vurugu kwa wadau wa mchezo huo wengine wakihoji sababu za wagombea wanane kati ya 12 kuenguliwa.

Miongoni mwa walioenguliwa ni  Suleiman Nyambui, Mohammed Kiganja na Rahim Kalyango waliokuwa wakiwania nafasi ya makamu mwenyekiti, huku Juma Ikangaa, William Kalaghe na Shaban Hiki wakipitishwa kwenye nafasi hiyo.

Kwenye ujumbe wa kamati ya utendaji wa kanda ya Pwani, Felix Chunga alipitishwa peke yake huku wengine watatu wakienguliwa.

Baada ya matokeo ya usaili, baadhi ya walioenguliwa waliandika barua Barua Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupinga mchakato.

Katibu mkuu wa BMT, Neema Msitha alikiri kupokea malalamiko hayo na jana msajili wa vyama vya michezo alikuwa na kikao cha muda mrefu na uongozi wa RT, kabla ya leo kutimuliwa ukumbini.

Wajumbe wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) wametimuliwa ukumbini dakika chache kabla ya kuanza mkutano mkuu na uchaguzi mdogo mjini Dodoma.

Mkutano na uchaguzi huo vilipangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Magereza, Msalato.

Ilipofika saa 4:20, wajumbe wakiwa ndani ya ukumbi ilitangazwa oda hawataki kuwaona.

"Hii imetoka kwa mkuu wa jeshi, hamtakiwi kuonekana hapa," alisema mwenyeji na kuondoka bila kutaka maswali.