AJ, Ruiz kuwabeba mabondia Watanzania

Muktasari:
Swedi ana rekodi ya kushinda mapambano 12, amepigwa mara sita na kutoka sare mara mbili, wakati Selemani ameshinda mapambano 20, amepigwa mara 15 na sare 5.
ENDAPO Swedi Mohammed na Selemani Said, mabondia wa Tanzania watakaozichapa kesho Jumamosi nchini Saudi Arabia kuwasindikiza Andy Ruiz Jr na Anthony Joshua watashinda mapambano hayo wataweka rekodi mbili kwa mpigo.
Anthony Joshua (AJ) na Ruiz Jr watazichapa pambano la marudiano la kuwania ubingwa wa World Boxing Association Super World (WBA), International Boxing Federation World (IBF), World Boxing Organisation World (WBO), International Boxing Organization World (IBO) kwenye uzani wa juu.
Awali mataji hayo yalikuwa yakishikiliwa na AJ kabla ya kuvuliwa na Ruiz Jr kwa kipigo cha TKO nchini Uingereza na kesho watarudiani kwenye ukumbi wa Diriyah Arena, mjini Diriyah, Saudi Arabia.
Pambano hilo litatanguliwa na mengine sita, manne yakiwa ya uzani wa juu huku Watanzania Swedi Moahmmed akizichapa kwenye uzani wa super bantam na Seleman Said akizichapa kwenye uzani wa kati.
Endapo watashinda mapambano hayo, Watanzania hao wataweka rekodi mbili kwa mpigo, kwanza kushinda kwenye pambano kubwa la dunia, lakini pia kuwachapa mabondia wenye rekodi ya kutopigwa.
Selemani atazichapa na Diego Pacheco mwenye rekodi ya kushinda mapmabno yake saba aliyokwishacheza na hajawahi kupigwa sawa na Ivan 'Hopey' Price ambaye atamkabiri Swedi.
Ivan licha ya kuwa chipukizi, amepigana pambano moja na hajawahi kupigwa, endapo atachapwa kesho itakuwa ni mara yake ya kwanza na Swedi ndiye atakuwa bondia wa kwanza kumchapa bondia huyo Muingereza anayetokea kwenye kambi ya AJ.
"Nimejiandaa vizuri, sina presha na pambano, nitamchapa Muingereza kama napiga punching bag, Watanzania waondoe wasiwasi na mimi na wanitizame kwa wingi kesho, nitakapokuwa namchaka Ivan," alisema Swedi kwa simu kutoka Saudi Arabia.
Selemani alisema hatofanya makosa kwenye pambano hilo, anahitaji kuvunja rekodi ya kutopigwa ya mpinzani wake, jambo ambalo analiona kwake si tatizo, yuko fiti na anatarajia ushindi kesho.