Aisha Masaka kuanza na Everton, Man City
Muktasari:
- Masaka alisajiliwa msimu huu na klabu hiyo akitokea BK Hacken ya Sweden alikodumu kwa misimu miwili tangu ajiunge nao mwaka 2022 akitokea Yanga Princess.
MSIMU mpya wa Ligi ya Wanawake England unaanza rasmi mwezi huu na klabu ya Brighton & Hove Albion anayoichezea Mtanzania, Aisha Masaka inatarajiwa kuanza na Everton Septemba 21.
Masaka alisajiliwa msimu huu na klabu hiyo akitokea BK Hacken ya Sweden alikodumu kwa misimu miwili tangu ajiunge nao mwaka 2022 akitokea Yanga Princess.
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo, Septemba 21 Brighton itaanzia nyumbani Uwanja wa Broadfield kisha wiki moja baadae kukipiga na Man City ugenini.
Baada ya michezo miwili ya ligi, Oktoba 02 timu hiyo itaanzia ugenini kwenye michuano ya FA hatua ya makundi dhidi ya Birmingham City ambayo Brighton imepangwa kundi D na Leicester City, Birmingham na Bristol City.
Msimu uliopita mshambuliaji huyo akiwa na Hacken aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kucheza michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) na sasa anakuwa Mtanzania pekee wa kwanza kuichezea Ligi Kuu England.
"Nimejiandaa kwenda kupambana kuhakikisha nafanikiwa kama ilivyokuwa Sweden, ni ndoto ya wachezaji wengi kucheza ligi kubwa kama England," alisema Masaka.