Ada ya usajili wachezaji wa kigeni yapanda

Muktasari:

Ligi Kuu Bara itaanza Septemba 6 na itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii utakaofanyika Agosti 29

Bodi ya Ligi na klabu za Ligi Kuu zimepitisha kanuni ikiwemo ya kuongeza ada ya usajili wa wachezaji wa kigeni kitoka Sh2 milioni hadi Sh4 milioni.

Makubaliano hayo yamefanyika leo katika kikao cha Bodi ya Ligi na klabu za ligi kuu kilichofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo amesema kikao cha leo kilikuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo kujadili mabadiliko ya kanuni na uendeshaji wa ligi.

"Lengo la kikao hiki ni kujadili mambo mbalimbali kabla ya ligi kuanza ili kuweza kuifanya ligi kuwa na ushindani”.

"Mojawapo mabadiliko ya kanuni ambayo klabu imepitisha ni ada ya usajili wa wachezaji wa kigeni kutoka Sh2 milioni za msimu uliopita na sasa klabu zitalipa Sh4 milioni kwa kila mchezaji”

"Pia kulikuwa na kanuni ya kuzitaka klabu kuwasilisha majina ya wachezaji wao na  benchi la ufundi wakati wa kikao cha maandalizi ya mechi na jambo hilo lilisababisha klabu nyingi kupata sana adhabu kwa kushindwa kufanya hivyo , sasa katika kikao cha leo tumeazimia kuwa sasa majina yatakuwa yanawasilishwa masaa mawili kabla ya mechi" amesema Kasongo.

Pia alisema msimu ujao mechi za katikati ya wiki zitapungua ili kutoa fursa kwa klabu kujiandaa na kusafiri bila presha kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.