7G yaipa Biashara United jeuri kwa Mbeya Kwanza

Muktasari:
- Biashara United ikiwa nyumbani mjini Musoma iliwakanda maafande hao kwa mabao 7-0 na kubaki nafasi yao ya pili kwenye Championship kwa pointi 53 baada ya michezo 25.
USHINDI mnono walioupata Biashara United juzi dhidi ya Ruvu Shooting, umeongeza nguvu na morali kikosini humo, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah akiipigia hesabu Mbeya Kwanza.
Biashara United ikiwa nyumbani mjini Musoma iliwakanda maafande hao kwa mabao 7-0 na kubaki nafasi yao ya pili kwenye Championship kwa pointi 53 baada ya michezo 25.
Kwa sasa timu hiyo inajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Mbeya Kwanza iliyo katika nafasi ya nne kwa alama 50 utakaopigwa wikiendi hii kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Mbeya Kwanza ambayo imetoka kushinda mabao 4-1 mbele ya Stand United inahitaji ushindi pia ili kujiweka kwenye hesabu za kurejea Ligi Kuu baada ya kuikosa misimu mitatu.
Josiah alisema ushindi huo uliwapa nguvu na mwanga wakati wakijiandaa na mchezo dhidi ya wapinzani hao, akikiri kuwa mechi hiyo inahitaji utulivu, nidhamu na akili nyingi kutoboa.
Alisema alikoshwa na kazi nzuri ya straika wake kwa kutumia vyema nafasi walizopata akieleza kuwa mbinu zilizotumika kuimaliza Ruvu Shooting zinaweza kuwa zaidi kwa Mbeya Kwanza.
“Kila mmoja anatekeleza majukumu yake, benchi la ufundi tuliridhishwa na matokeo hayo ambayo yanatupa nguvu kukiandaa kikosi dhidi ya mechi ngumu ijayo,” alisema na kuongeza:
“Tunajua wapinzani wapo nyumbani na kila mmoja anahitaji pointi tatu, lakini tutaenda kwa kuwaheshimu, tukitumia akili ili kuondoka japo na pointi moja kama tatu zitagoma,” alisema Josiah.
Aliwataka wachezaji kutobweteka na matokeo ya mechi iliyopita bali kupambana kwa tahadhari na kutumia nafasi watakazopata ili kuendelea kuwa kwenye mbio za kupanda Ligi Kuu.