300 washiriki mazoezi ya Yoga Arusha

Muktasari:

  • Washiriki hao wamejitokeza katika maadhimisho ya siku ya Yoga duniani lengo ikiwa ni kuboresha afya na ustawi wa mwili lakini pia kama nyenzo ya kukabiliana na magonjwa mbali mbali ikiwemo msongo wa mawazo, presha na kisukari 

Zaidi ya washiriki 300 kutoka maeneo mbali mbali ya jiji la Arusha wamefanikiwa kushiriki mazoezi maalum ya Yoga huku wakitaka jamii zingine kuifanya kama desturi katika ratiba zao za kila siku kujinga na magonjwa na msongo wa mawazo.

Mazoezi hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa ‘Fun Retreat’ yaliandaliwa na ubalozi wa kudumu wa India kwa lengo la kuadhimisha siku ya kimataifa ya Yoga duniani.

Akizungumzia mazoezi hayo, Kishen Majithia alisema kuwa mazoezi ya Yoga yanasaidia kuboresha afya na ustawi wa mwili lakini pia kama nyenzo ya kukabiliana na magonjwa mbali mbali ikiwemo msongo wa mawazo, presha na kisukari endapo yakifanyika kila siku asubuhi mara baada ya kuamka.

“Yoga ni mfumo wa zamani wa mazoezi ya viungo, akili na nafsi ambao ulianzia India na sasa unafanyika duniani kote na tunaadhimisha kila june 21, hivyo jamii ione umuhimu wa kufanya mazoezi haya kila siku asubuhi angalau dakika 15 kabla ya kuanza ratiba ya siku hakika wataona mabadiliko makubwa katika miili yao na akili pia”

Alisema kuwa wako katika mipango ya kuanzisha madarasa ya Yoga maeneo mbali mbali mkoani Arusha ili kufundisha jamii namna bora ya kufanya mazoezi hayo yalete tija katika miili yao lakini pia kuwapa fursa wageni wa kimataifa wanaofika Arusha kupata pa kufanyia mazoezi.

Akizungumza baada ya kufanya mazoezi hayo, Mea wa jiji la Arusha Maximillian Iranghe alisema kuwa Yoga imekuwa msaada mkubwa kwa jamii ya kihindi wanaofanya kazi mkoani Arusha hivyo kuwataka watanzania waige mfano huo kwa uchumi imara na endelevu wa jiji kwa kuepuka magonjwa.

“Mimi nimekuwa nikishangaa wenzetu wahindi wanadumu miaka nenda rudi kwenye biashara na maduka yao bila kuumwa hovyo kumbe siri ni mazoezi haya ya Yoga ambayo wamesema kila siku asubuhi ni desturi yao kufanya angalau dakika 15, aisee na sisi watanzania tuige hii”

Mea Iranghe alitumia nafasi hiyo kuiomba kamati ya Olympiki nchini kupelekea ombi maalum ya kuuongeza Yoga katika mashindano yao ili kufanya hamasa kwa jamii zingine kufanya mazoezi.

Kwa upande wake mmoja wa wadhamini wa mashindano, Abubakari Omary alisema kuwa wanatarajia kufanya matamasha mengi zaidi ya Yoga ili kutoa hamasa kwa watanzania wengi kushiriki na kunufaika nao.