100 washiriki mchezo wa gofu kuadhimisha miaka 50 ya Tazara
Muktasari:
- Akizungumza wakati wa mchezo huo uliofanyika viwanja vya Lugalo mwishoni mwa wiki, Nahodha gofu klabu ya Lugalo, Paul Mosha, amesema awali wakati wanatangaza kuwepo kwa mchezo huo walitarajia kupata wachezaji 100, lakini imekuwa tofauti kutokana na mwitikio mkubwa walioshiriki ni zaidi ya hiyo namba.
Zaidi ya wachezaji 100 wamejitokeza kwenye mchezo wa gofu ,ikiwa ni shamrashamra za kusheherekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia(Tazara).
Akizungumza wakati wa mchezo huo uliofanyika viwanja vya Lugalo mwishoni mwa wiki, Nahodha gofu klabu ya Lugalo, Paul Mosha, amesema awali wakati wanatangaza kuwepo kwa mchezo huo walitarajia kupata wachezaji 100, lakini imekuwa tofauti kutokana na mwitikio mkubwa walioshiriki ni zaidi ya hiyo namba.
Mosha amesema wamefurahi Tazara kuuchagua mchezo huo katika maadhimisho yao jambo ambalo linadhihirisha kuwa mchezo huo kwa sasa unakua.
"Kwa nini mchezo wa gofu unakuwa,Tazara inatoa huduma kwa zaidi ya miaka 50 sasa na inawahudumia watu, hivyo na huku kwenye gofu itawakuta watu wa kutosha.
"Kwa hiyo Tazara imethamini mchezo wa gofu na ndio maana imeamua uwe mmoja wa michezo katika maadhimisho hayo ya miaka 50 ,"amesema.
Hata hivyo ili mchezo huo uendelee kukubalika na watu Mosha ameshauri wachezaji waandaliwe tangu wakiwa wadogo kwa kuwa ni rahisi kushika sheria zake na pia ni wepesi kunyumbulika katika kuucheza tofauti na mchezaji akiwa mtu mzima.
Nahodha huyo ameongeza kuwa tayari katika klabu hiyo wana watoto takribani 100 ikiwa ni tofauti na miaka ya nyuma watoto walikuwa hawafiki hata 20.
Pia ameshauri katika shule kuangalia namna gani wanaweza kuwa na maeneo makubwa yatakayowezesha kuwa na mchezo huo pia ili iwe rahisi kwa wanafunzi kujifunza.
"Gofu inatengeneza maisha na hata ukiangalia wachezaji wakubwa wa mchezo huu wana maisha mazuri, hivyo tusiupuuze,"amesema Mosha.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia(TAZARA), Bruno Chinga'andu, amesema wamefurahi kuungana na wanamichezo hao kisheherekea maadhimisho hayo ya miaka 50 ya Mamlaka.
Chinga'andu amesema Tazara wakati huo ikijulikana kama Shirika la reli, lilianzishwa miaka ya 76 ikiwa ni wazo la baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Rais wa Zambia,Kenneth Kaunda.
"Wakati Tazara inaanzishwa ,Zambia ilikuwa imefungiwa mipaka yake hivyo ikawa kama moja ya njia ya kuikomboa nchi hiyona nyingine za Afrika kutoka mikononi mwa wakaloni.
"Ikiwa imefikisha miaka 50,amesema malengo ni kuona reli ya Tazara inajiendesha kibiashara zaidi,amesema Mkurugenzi huyo.
Kuhusu kuchagua mchezo wa Gofu katika maadhimisho hayo, Chinga'andu, amesema huko pia kuna wafanyabiashara wengi hivyo ni moja ya njia ya Tazara kukutana nao na kuweza kufanya mazungumzo ya kibiashara pia.