Zoran: Kwa mziki huu, mmeumia

KIKOSI cha Simba kimetua jananchini Misri na wachezaji wakafanya mazoezi kwa awamu ya kwanza wakiwa katika ardhi hiyo kama maandalizi ya msimu ujao, huku kocha wa timu hiyo, Zoran Maki akichekelea usajili uliofanywa akisema; ‘Wameumia’.
Zoran aliyeajiriwa hivi karibuni kwa mkataba wa mwaka mmoja, alisema usajili uliofanywa hadi sasa unampa picha atakuwa na timu kali ambayo itasumbua kwenye msimu ujao wa mashindano kuanzia Ligi Kuu Bara, ASFC hadi michuano ya kimataifa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zoran alisema amemfuatilia Moses Phiri anayetokea Zambia na kusema ni moja ya wachezaji wazuri mwenye uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga, kufunga mwenyewe na ndani ya msimu mmoja anaweza kufunga si chini ya mabao kumi.
Alisema uwepo wa Phiri katika kikosi chake utampa nafasi ya kumtumia kutokea pembeni kushoto au kulia, nyuma ya mshambuliaji au hata kwenye kiungo na kote anaweza kufanya vizuri kutokana na uwezo wake.
“Nimefuatilia Ligi Kuu ya Ghana nimemuona vizuri huyo Augustine Okrah ni aina ya mchezaji mwenye kipaji si katika kushambulia tu bali anawasumbua hata mabeki wa timu pinzani,” alisema Zoran na kuongeza;
“Uwepo wa Okrah katika kikosi chetu na kama atacheza kwenye kiwango nilichomuona akiwa ndani ya timu yetu nina imani utakuwa moja ya usajili mzuri kutokana na uwezo alionao.
Okrah anapokuwa na mpira mguuni anaweza kufanya matendo sahihi kwa maana ya kupiga pasi za mwisho, kutengeneza shambulizi na kufunga mwenyewe mabao kwa aina mbalimbali.”
Zoran aliongeza kwa kusema; “Niliangalia mechi mbalimbali za mashindano ya ndani ikiwemo ile fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), huyo Victor Akpan alicheza vizuri kama nilivyoonyeshwa mechi mbili za ligi dhidi ya Simba.
“Kuhusu wachezaji wa ndani Nassoro Kapama na Habib Kyombo nitakwenda kuwaona zaidi katika kambi yetu Misri. naamini hadi kusajiliwa Simba wana uwezo wa kuipigania timu na wakafanya vizuri.”
Baada ya kuwatambulisha nyota hao Simba ikiwa Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao (Pre-season), itaweka wazi mashine nyingine mpya tatu, Cesar Lobi Manzoki, Nelson Okwa na Mohamed Ouattara.Aidha, Zoran alisema katika maandalizi hayo hatakuwa na wachezaji wote kutokana na wengine watano kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambao ni Aishi Manula, Kennedy Juma, Mohammed Hussein, Mzamiru Yasin na Kibu Denis.
“Hadi wakati huu sijafahamu kama nyota hao nitakuwa nao kwenye kambi Misri, ila naelewa kuna wachezaji wengine tutaungana nao huko huko kwa ajili ya maandalizi yetu,” alisema Zoran.