Zidane ataka Messi asiondoke Barcelona

Madrid, Hispania. Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amemtaka mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi kubaki kwenye timu hiyo licha ya kwamba mchezaji huyo ni muhimu kwelikweli kwa wapinzani wao.

Messi ameripotiwa kuwa na mpango wa kuachana na miamba hiyo ya Nou Camp, Barcelona, wakati mkataba wake utakapofika tamati 2021 baada ya kutibuana na klabu hiyo.

Mshindi huyo mara sita wa tuzo ya mchezaji bora duniani ‘Ballon d’Or’ anaripotiwa kwamba hafurahii maisha ya sasa Barcelona kutokana na kulaumiwa mara kwa mara pale mambo yanapokwenda kombo kikosini.

Lakini, kitu cha kushangaza ni kwamba kocha wa Real Madrid, Zidane, hataki Messi aondoke licha ya uwepo wake kuwa tatizo kikwazo kwa timu yake katika kubeba mataji ya La Liga kila mwaka.

Zidane alisema La Liga inapaswa kupambana kuwabakiza wachezaji wake muhimu wasiende kwenye ligi zingine barani Ulaya.

“Sijui nini kitatokea kwa sababu haitakuwa kwa sababu yupo kwenye ligi na sisi tunataka ubora kwenye hii ligi,” alisema Zidane baada ya Real Madrid kuichapa Getafe bao 1-0, juzi.

Katika mchezo huo, Sergio Ramos alifunga bao pekee kwa mkwaju wa penalti. Ushindi huo umeifanya Real Madrid kujitanua zaidi kileleni kwenye msimamo wa ligi dhidi ya Barcelona.

Zidane alimzungumzia Ramos akisema, “ni nahodha wetu, kiongozi wetu ndani na nje. Ni mchezaji wa aina yake.”