Yanga yataka mabeki wawili jeshini
Muktasari:
- Yanga imeweka kambi kwenye kikosi cha Mashujaa ikianza na beki wa kati Mohammed Mussa, ikimpa ofa kubwa ya kumsajili kwa hesabu za msimu ujao.
Yanga inapambana kukamilisha usajili wa wachezaji wawili walioitumikia timu moja ya jeshi, Mabingwa wa Ligi Kuu Bara wakiendelea na msako wa kuimarisha kikosi chao.
Yanga imeweka kambi kwenye kikosi cha Mashujaa ikianza na beki wa kati Mohammed Mussa, ikimpa ofa kubwa ya kumsajili kwa hesabu za msimu ujao.
Awali Yanga ilikuwa na hesabu za kumsajili beki Nasri Kombo ambaye ni nahodha wa TRA United, kabla ya mazungumzo hayo kuzorota hivi karibuni na kutua kwa Mussa.
Mussa amekuwa beki muhimu wa Mashujaa msimu huu akicheza mechi 25 kati ya 30,akionyesha uwezo mkubwa wa kukaba kwa nguvu.
Yanga hata hivyo hata kama itamalizana na Mussa bado italazimika kumalizana na Mashujaa kutokana na beki huyo bado ana mkataba wa miaka miwili na wanajeshi hao.
Mbali na Mussa pia Yanga inataka kumsajili beki wa kulia Abdulnassir Assa 'Gammal' kutoka hapo hapo Mashujaa.
Yanga inataka kumuongeza Gammal kwenye nafasi ya beki wa kulia ambapo Mwanaspoti linafahamu kuwa ndiye atakuwa mrithi wa Israel Mwenda ambaye ataachwa.
Mwenda alikacha kuendelea na Yanga ikielezwa alitoweka bila kutoa taarifa huku mabosi wa klabu yake wakibariki uamuzi huo kufuatia mahusiano ya pande hizo mbili kupata shida.
Licha ya Gammal kukubali kutua Yanga lakini mabosi wa Mabingwa hao tena watalazimika kukaa mezani na wenzao wa Mashujaa ili wamalizane.