Yanga, SportPesa na tafsiri ya sheria

Dar es Salaam. Vuguvugu la kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mdhamini wake mkuu, SportPesa limezidi kukolea baada ya wanasheria wakitofautiana juu ya sakata hilo.

Yanga na Sportpesa zilianza kuvutana mwanzoni mwa wiki hii kutokana na Yanga kuingia mkataba na kampuni ya Haier kama mdhamini mkuu kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga na SportPesa kwa nyakati tofauti walitoa matamko yao, huku kila mmoja akionekana kuvutia upande wake.

Akizungumzia saka hilo baada ya Yanga kutoa tamko juzi, mwanansheria Frank Chacha alisema Yanga ilitakiwa ipate ridhaa kutoka kwa SportPesa kabla ya kusaini mkataba na wadhamini wengine kwa sababu tayari ina mdhamini mkuu.

Chacha alisema kwa upande wa Yanga kukataliwa na CAF kuitumia SportPesa kwenye mashindano yao ni sahihi kikanuni, lakini kama kampuni hiyo ndiyo wadhamini wakuu kwenye ligi zote ambazo timu inashiriki, ilitakiwa ikae chini na kushauriana nini cha kufanya kimataifa.

“Kama mkataba wa Yanga na SportPesa una kipengele cha Absolute Rights (mipaka ya kimkataba), basi wadhamini (Sportpesa) hawana haki, lakini kama ndiyo wadhamini wakuu (Sportpesa) kote na hakuna wanapobanwa kwenye mkataba wao, basi ilitakiwa wakae chini.

“Hata kama Sportpesa haitumiki Caf, ila ni wadhamini wakuu wa Yanga kwenye mashindano yote kama wamesaini hivyo, wangekaa chini na Yanga ingewaambia kuna mdhamini mwingine na ingeangaliwa kiasi cha fedha halafu wanasaini kwa sababu wote ni wafanyabiashara,” alisema Chacha.

Mwanasheria maarufu, Alex Mgongolwa alisema kwa upande wake anaona SportPesa inapotoka kwenye tafsiri ya dhana kwa sababu kanuni ndiyo imeibeba Yanga kupitia Caf.

“Yanga iliijulisha Sportpesa kuhusu mdhamini mwingine ili isishangae, wao kuipa Yanga jina la Visit Tanzania kutumia kwenye mechi hiyo huku ikiwa si wamiliki wa nembo hiyo kuikosea Yanga.

“Wenye haki na neno lile ni Wizara ya Utalii na si ya kwao, wao nembo zao mbili zote zimekataliwa na Caf kwahiyo unaona kabisa hata ile ya pili kama Yanga ingesema iitumie tu basi wangeweza kuumizwa na Caf,” alisema Mgongolwa.