Yanga: Jidanganyeni tu

MASHABIKI wa Simba wamepandwa na mzuka baada ya gepu la pointi dhidi ya Yanga kupungua kutoka 12 hadi nane na wamekuwa wakiwatambia wenzao wa Jangwani kuwa wanabeba ndoo ya tano mfululizo, lakini nahodha wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara, Bakari Nondo Mwamnyeto amewaambia wanajidanganya.

Mwamnyeto amesema ubingwa msimu huu ni Yanga akisisitiza kuwa wapo Dodoma kuchukua pointi tatu katika mechi yao ya Jumapili dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri.

“Tunahitaji kuondoa gundu la droo kwenye mechi tatu mfululizo, hivyo tunakwenda Dodoma na nguvu na ari mpya ya kupata matokeo mazuri,” alisema.

Kuhusu walichokiboresha kwenye kikosi chao baada ya sare mfululizo, Mwamnyeto alisema kilichotokea ni upepo tu.

“Katika maisha kuna wakati wa raha na shida, hata maandiko matakatifu yanatueleza hivyo, Yanga tulipitia kwenye raha, sasa ni wakati wa shida lakini naamini tutatoka hapa tulipo na kuwa kwenye raha zaidi siku si nyingi,” alisema.

Kuhusu safari ya ubingwa, mchezaji huyo alisema kutokana na tofauti ya pointi walizonazo mpaka sasa, ubora wa kikosi chao na hamasa ya timu, kombe ni lao msimu huu.

“Ubingwa bado huko wazi kwa Yanga, pointi nane sio ndogo, na tunaahidi tunakwenda  kupambana kurejea na pointi tatu,” alisema.


KISAIKOLOJIA ZAIDI

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay na kocha wa zamani wa timu hiyo, Kenny Mwaisabula, wanaamini wachezaji wa Yanga wakisaidiwa kisaikolojia tu wanabeba ndoo hiyo waliyoipoteza mikononi mwa mahasimu wao Simba kwa misimu minne mfululizo.

Mayay alisema Yanga imethibitisha kuwa ni timu bora tangu mwanzo wa msimu huu na tatizo lililowakabili katika mechi tatu zilizopita ni maandalizi ya kisaikolojia tu kwa wachezaji wao hadi mashabiki na uongozi pia.

“Mchezo dhidi ya Prisons umewafanya Yanga presha izidi kupanda, maana presha ilikuwa kubwa sana na hasa ikizingatia nafasi ya Prisons kwenye msimamo, na sasa wanazidiana na Simba alama nane hapo ndipo wanapozidi kuchanganyikiwa.

“Wachezaji nao waondoe fikra ya kwamba ni lazima staa wao Fiston Mayele afunge. mfano katika mchezo uliopita Saido Ntibazionkiza alipata nafasi na hata Feisal Salum alipata nafasi, lakini akili zao zote zinahitaji afunge Mayele, sasa hilo litazidi kuwatesa sana, mechi ijayo wanacheza nje ya Uwanja wa Mkapa na kiwango cha timu hiyo inapokutana na Simba na Yanga sio mchezo. Ni lazima waonyeshe ukomavu,” alisema Mayay.

Mwaisabula alisema: “Presha ni kubwa na hakuna namna nyingine zaidi ya Yanga kushinda mechi ijayo na Dodoma ili kutengeneza mazingira mazuri ya ubingwa.”

Alisema kwa hali ilivyo sasa, kama ligi ingekuwa bado ni ndefu lolote lingeweza kutokea, lakini kwa michezo iliyosalia, Yanga wana kila sababu ya kutwaa ubingwa.