#WC2018: Suarez aumia mazoezini, Cavani ajiuguza

Muktasari:
- Habari mbaya ni kwamba, wakati Cavani akiendelea kujiuguza, pacha wake katika safu ya ushambuliaji, Luis Suarez, naye anaripotiwa kuumia mazoezini. Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa leo, ni kwamba nyota huyo wa Barcelona alilazimika kuchechemea akitoka uwanjani, baada ya kupata maumivu kwenye mguu wa kulia.
Moscow, Russia. Ni kama bundi mweusi ametua katika kambi ya Uruguay. Baada ya kuifungisha virago Ureno, Uruguay ilijikuta ikimpoteza Straika wake Edison Cavani, aliyepata jeraha baada ya kutupia wavuni mara mbili katika ushindi wa 2-1.
Habari mbaya ni kwamba, wakati Cavani akiendelea kujiuguza, pacha wake katika safu ya ushambuliaji, Luis Suarez, naye anaripotiwa kuumia mazoezini. Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa leo, ni kwamba nyota huyo wa Barcelona alilazimika kuchechemea akitoka uwanjani, baada ya kupata maumivu kwenye mguu wa kulia.
Uruguay inaendelea na mazoezi katika uwanja wa Nizhny Novgorod, iliko kambi yao kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wa robo fainali dhidi ya France, iliyofuzu kwa kuifunga Argentina 4-3 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano.
Hata hivyo, taarifa hizo zinaelewa kuwa, Suarez aliweza kuendelea na mazoezi, lakini anaonekana kutokuwa vizuri kifiziki ba kisaikolojia. France inayonolewa na Didier Deschamps itakutana na Uruguay ya Oscar Tabarez katika mechi ya robo fainali, itakayopigwa siku ya Ijumaa.