#WC2018: Ramirez aachia ngazi huko Costa Rica

Moscow, Russia. Siku chache baada ya kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Russia, katika hatua ya Makundi na Brazil, Kocha wa Costa Rica, Oscar Ramirez ametangaza kubwaga manyanga.
Costa Rica, ambao walitinga robo fainali ya michuano, miaka minne iliyopita huko Brazil, walijikuta wakishindwa kutamba mbele ya vijana wa Tite, waking'olewa kibabe, wakimaliza mechi za kundi E, wakiwa na pointi moja tu.
Juni 25, baada ya kubanwa na Switzerland ambapo walitoa sare ya 2-2, Oscar Ramirez ambaye alichukua majukumu ya kuongoza kikosi cha Costa Rica, mwanzoni mwa mwaka 2015, alinukuliwa akisema kuwa hana uhakika kama ataendelea kubaki katika nafasi yake.
Kauli hii, ilikuja kutimia jana ambapo Rais wa shirikisho la Soka la Costa Rica, Rodolfo Villalobos, alithibitisha kwamba, Kocha huyo mwenye umri wa miaka 53, ameomba kupumzika ombi ambalo, uongozi wa Soka umeridhia na kuongeza kwamba mkataba wa Kocha hautaongezwa.
"Oscar Ramirez, hataongezewa mkataba. Ameomba kupumzika na sisi kama uongozi wa soka tumeridhia, baada ya mechi ya Switzerland tuliongea kwa kirefu, na tumekubaliana kuwa Ramirez hatokuwa sehemu ya maandalizi yetu kuelekea Qatar 2022," alisema Villalobos.