Vichwa 9 vyaipa jeuri Yanga SC

KASI ya Yanga inawapa jeuri kubwa mashabiki wa klabu hiyo mtaani. Asilimia kubwa wanaamini msimu huu timu hiyo inabeba ndoo zote mbili, kuanzia ile ya Kombe la Shirikisho (ASFC) hadi ya Ligi Kuu Bara.
Jeuri hiyo inatokana na awali chama lao kubeba Ngao ya Jamii kwa kuifumua Simba kwa bao tamu la Fiston Mayele, lakini hata kwenye ASFC timu hiyo ipo robo fainali na katika Ligi Kuu inaoongoza msimamo kibabe ikiwa na pointi 45.
Lakini imeibainika nyuma ya mafanikio yote ya Yanga msimu huu kuna vichwa tisa vinavyorahisisha mambo na kuifanya timu hiyo iwanyime raha Simba wanaopambana kutetea taji kwa msimu wa tano mfululizo.
Ni kweli sifa nyingi zipo kwa timu nzima ikiwamo wachezaji na makocha wao, lakini kuna vichwa nane vyenye rekodi nzito zinazoipaisha Yanga kwa kusimamia ushindi na kila mipango kwa timu hiyo.
Nyuma ya ubora wa Yanga ukiondoa mastaa wao na makocha kuna tajiri wao namba moja Ghalib Said Mohamed ‘GSM’, lakini kama haitoshi jamaa akishirikiana na Mwenyekiti wa klabu, Dk Mshindo Msolla waliunda kamati nzito ya mashindano ambayo kimyakimya imekuwa ikihakikisha kila kitu kinakuwa sawasawa kupata ushindi nyumbani na ugenini.
Yanga msimu huu imetoa sare mbili tu katika mechi zao 10 za ugenini dhidi ya Namungo na ile ya Simba, huku nane ikishinda na utamu zaidi, ikishinda mechi zote ngumu zilizowatibulia msimu uliopita dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania.
Chini ya Mwenyekiti wake, Rodgers Gumbo akiwa na wajumbe wake wanane, kamati hiyo imekuwa ikipambana katika kila mchezo kuhakikisha kikosi chao kinaingia uwanjani kushinda kwa ubora huku makosa yakibaki kwa marefa tu.
Mbali na Gumbo, wajumbe wa kamati hiyo ni; Hamad Islam, Abdallah Bin Kleb, Davis Mosha, Lucas Mashauri, Seif ‘Magari’ Ahmed, Injinia Hersi Said, Arafat Haji na Pelegrinius Rutayuga.
Kwa sasa kamati hiyo imekuwa ikimtanguliza mbele Hersi, ambaye amekuwa akipaa na kikosi hicho kuanzia inapoanza safari na hata kurudi nayo huku Gumbo akiwa nyuma yake kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.
Nyuma ya Hersi vigogo wengine wamekuwa wakipambana msituni huku wakitua katika mechi zao siku moja kabla ya mchezo kuhakikisha wanashuhudia ushindi unapatikana.
Pale Tanga wakati Yanga inaipiga Coastal mbali na Hersi ambaye anasifika kwa kujua kupiga hesabu kali za kuwahamasisha wachezaji aliungana na Gumbo, Mosha huku kigogo mwingine wa nje ya kamati hiyo Frank Kamugisha akiwa mkuu wa msafara kutoka kamati ya utendaji na Yanga ikapindua meza na kushinda kwa mabao 2-0.
Itakumbukwa vigogo wengi wa kamati hiyo wamekuwa na rekodi nzito za kuipigania Yanga ambapo Bin Kleb mkasa wake mkubwa aliifanyia Simba umafia mkubwa akimnyakua beki Mbuyu Twite na kuiacha Simba solemba.
Achana na mkasa huo yupo pia kiungo Feisal Salum ambaye alishasaini Singida United, Kleb akishirikiana na Mashauri walipindua meza kisha kumsainisha na kupindua meza katika dili hilo.
Islam, Mosha, Magari na Bin Kleb wanakumbukwa vyema jinsi walivyotoa mchango mkubwa kwa Yanga kuipokonya Simba tonge mdomoni katika msimu wa 2016/2017 ambapo Wekundu waliongoza kwa pointi 11, lakini kombe likaenda Yanga.