Utulivu mechi ya Yanga, Simba watawala

HALI ni shwari, ndivyo unavyoweza kusema kwa mashabiki wa Yanga, Simba waliohudhuria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Timu hizo zinakutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii huku kila shabiki akionyesha kuwa na imani kubwa ya kushinda kwenye mechi ya leo.

Mbali na mashabiki hao kutambiana kabla ya mchezo huo inaotarajiwa kupigwa saa 1:00 usiku ila hali ya usalama ni shwari huku mashabiki waliohudhuria wakifuata utaratibu vizuri wakati wa kuingia.

Jeshi la Polisi nao hawako nyuma kufanya doria kwenye maeneo mbalimbali nje ya uwanja ili kuhakikisha wanalinda usalama wa raia na mali zake.

Yanga na Simba zinakutana huku kila shabiki akijivunia kikosi imara kutokana na usajili uliofanyika.

Mashabiki wa Yanga wameonyesha imani kubwa na kiungo wao mshambuliaji Stephane Aziz KI aliyesajiliwa kutokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast huku kwa upande wa Simba wakijivunia usajili wa Augustine Okrah aliyeyokea Bechem United ya Ghana.



Mashabiki wajivuta kuingia uwanjani

IKIWA yamebakia masaa kadhaa kabla ya mechi hiyo kupigwa katika uwanja wa mkapa, Jijini Dar, ni mashabiki wachache tu hadi sasa ambao wameonekana kwenye foleni ya kuingia Uwanjani.

Mwanaspoti ilifika uwanjani hapo na kuzunguka kwenye mageti yote na kushuhudia kwamba kuna idadi ndogo ya mashabiki waliopanga foleni ya kuingia uwanjani tofauti na ilivyozoeleka hasa katika masaa ya mwisho.


Mbali ya sehemu ya kuingilia, Mwanaspoti pia ilifika sehemu wanayokatisha tiketi ambapo pia hakuna watu wengi.
Mashabiki walianza kuingia Uwanjani tangu asubuhi kwa ajili ya kutazama mechi hiyo ambayo itaanza saa 1:00 usiku.