Ulimwengu kalianzisha tena huko TP Mazembe

Thursday January 14 2021
ulimwengu pic
By Mwandishi Wetu

NANI aliyekuambia Thomas Ulimwengu amefulia? Moto alioanza nao kwa sasa ndani ya TP Mazembe, umemfanya kocha wa timu hiyo, Kazembe Mihayo kukiri jamaa kwa sasa karudi upyaa na atawasumbua sana wapinzani kwao katika ligi ya nyumbani na ile ya kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mihayo aliyekuwa nchini na timu ya taifa ya DR Congo iliyocheza na Taifa Stars na kutoka sare ya 1-1, alisema Ulimwengu ameanza msimu akiwa na kiwango bora ikitokana na jinsi walivyomtengeneza na kumrudisha kwenye ubora wake tofauti na alivyofika kwao.

Mihayo alisema wakati Ulimwengu akirejea Mazembe alilazimika kufanyiwa programu maalum ya kumpunguza uzito na sasa yuko sawa na ndio siri ya kufunga mabao mengi.

Mpaka sasa, nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania amefunga mabao manne katika mechi za Ligi Kuu ya DR Congo, lakini pia kasi yake hiyo haikusimama kwani katika Ligi ya Mabingwa Afrika amefunga mabao matatu, huku timu yake ikitinga hatua ya makundi.

“Alipofika hakuwa sawa kule alikokwenda hawakumtunza kama alivyokuwa Mazembe, alifika akiwa ameongezeka uzito sana tukalazimika kumpa programu maalum ambayo ilimsaidia kupungua kwa kiasi kikubwa,” alisema Mihayo aliye kocha msaidizi wa timu ya taifa hilo.

“Mnaona sasa anafanya vizuri kwa kuwa yuko sawa, nafurahia kazi yake ni mchezaji ambaye namfahamu vizuri anajituma sana na anapambana sio rahisi kuona anakata tamaa naona msimu huu atafanya vizuri sana,” alisema Mihayo na kuongeza; “Siku zote unapokuwa na mchezaji ambaye mlimlea na akarudi kisha akawa anafanya vizuri timu nzima mtafurahia, nafikiri mnafahamu kwamba Ulimwengu akiwa Mazembe ni kama yuko nyumbani.”

Advertisement
Advertisement