UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Simba warushe taulo tu uwanjani

Muktasari:

  • Singida Fountain Gate na Ihefu wala hawana woga tena wanapocheza na Simba. Sio jambo zuri kwa timu kubwa. Sio jambo zuri kwa timu ambayo malengo yake ni kutwaa Ubingwa.

SIMBA imekuwa na msimu mbaya. Taratibu inaanza kupoteza sifa ya kuwa mshindani namba moja wa Yanga. Taratibu inaanza kuzoea mazingira ya kumaliza msimu bila taji kubwa. Kitendo cha kucheza mechi tano za mwisho mfululizo kwenye michuano yote bila ushindi ni tabia ya timu ndogo. Kwa ukubwa wa Simba, hutarajii kuona wakicheza mechi tano bila kushinda hata moja.
Hii sio tabia ya timu kubwa. Kufungwa na Yanga mechi mbili za ligi sio jambo kubwa. Idadi ya mabao, pengine ndiyo kubwa zaidi. Ni kama Simba sasa imekuwa mnyonge dhidi ya Yanga. Wanajipigia tu.                            

Singida Fountain Gate na Ihefu wala hawana woga tena wanapocheza na Simba. Sio jambo zuri kwa timu kubwa. Sio jambo zuri kwa timu ambayo malengo yake ni kutwaa Ubingwa.
Simba msimu huu imefungwa mabao 7-2 na mtani wake, Yanga - idadi kubwa kama hii kwenye mechi za dabi haiji kwa bahati mbaya.


Kuna mahali Simba hawapo sawa. Kuna ubora umepungua. Kuna mahali Yanga wako juu. Kuna mahali Yanga wamepata namba za siri za kufungua kabati la Simba.
Ili kuendelea kuwa timu kubwa, ni lazima ushinde mataji makubwa. Ni lazima usonge mbele kwenye michuano mikubwa.

Ukiitazama Simba ya sasa kila mtu anaona namna timu inavyokwenda kwa kubahatisha.
Eneo la ushambuliaji inabahatisha. Eneo la kiungo nako tabu tupu. Simba imepoteza makali. Sio tena yule mnyama mkali. Eneo la ulinzi haieleweki. Kipa naye ni kama amevurugwa.

Kumekuwa na mashabiki wengi wanaodhani viongozi wakubwa wa Simba ni muda muafaka kwao kujiuzulu kwenye klabu hiyo. Labda mashabiki hao wana hoja ya msingi. Wasikilizwe. Labda pia mashabiki hao hawana hoja yotote isipokuwa  mihemko tu ya kufungwa na mtani na kufanya vibaya kiujumla msimu huu.

Kimahesabu, bado Simba inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, lakini kiuhalisi nafasi ni kama ngamia kupenya kwenye tundu la sindano. Mashabiki lazima wachanganyikiwe tu. Shida kubwa ya Simba nayoiona iko zaidi kwenye uwekezaji wa wachezaji bora. Tatizo la uongozi hata likitatuliwa haliwezi kuwapa Simba alama tatu uwanjani.

Ukishakuwa na wachezaji bora kwenye timu pale Simba hakuna kiongozi mbaya. Ukitazama Simba ilivyocheza hasa kwenye mechi zake tano za hivi karibuni unatamani kurusha taulo. Kanuni za ndondi ziko wazi kama unaona bondia wako hatoboi ulingoni ni bora kurusha taulo ili kumaliza pambano. Kunahitajika mabadiliko makubwa kuelekea msimu ujao.

Mashabiki wanapaswa kutulia na kuwapa nafasi viongozi ya kuandaa timu. Simba sio timu ya kwanza duniani kukosa mataji makubwa kwa msimu wa tatu mfululizo. Simba sio timu ya kwanza kuteseka. Ndiyo mchezo wa mpira wa miguu ulivyo. Migogoro ndiyo itawaondoa kabisa mchezoni.

Imewachukua Yanga msimu minne kuipata timu bora tunayoiona kwa sasa. Ulikuwepo uongozi wa Dk Mshindo Msolla haukufanya lolote. Ukaanza uongozi wa Hersi Said na mateso yake. Pamoja na mateso makubwa, lakini Yanga walibaki wamoja. Ndiyo unaona leo hii wanakula wali kwa mrija.

Timu haijengwi mara moja. Miongoni mwa makosa makubwa yaliyofanyika hivi karibuni pale Simba ni kuwaondoa Moses Phiri na Jean Baleke.
Baleke ameondoka Simba akiwa mfungaji bora. Muda huu angekuwa mbali na kimahesabu mabao yake yangesaidia kuongeza pointi. Kucheza mechi tano mfululizo bila kushinda mechi hata moja sio tabia ya timu kubwa. Simba inapaswa kutoka huko.

Mashabiki na wapenzi wanataka kuiona timu yao inarejea kwenye ubora na kuleta ushindani wa kweli. Mambo ya kufungwa na mtani mechi mbili mabao 7-2 huo sio utani wa jadi. Huu ni udhalilishaji wa jadi. Simba hakuna wanaloweza kufanya kwa sasa isipokuwa ni kutengeneza timu. Moja kati ya maeneo waliyopatia ni lile la ufundi.

Pamoja na kutopata matokeo mazuri,  lakini haiondoi ukweli kuwa Benchikha ni bonge la kocha. Fundi wa mbinu na mjuaji wa mechi aliyekosa wachezaji sahihi. Huyu Simba wanatakiwa kumng’ang’ania, wakimpa wachezaji wazuri na muda ana uwezo wa kurudisha makali ya mnyama. Kwa wachezaji hawa wa sasa cha kusaidia ni kutupa taulo stejini. Yanga wamejipata. Kwa sasa dabi inatabirika. Ukiwa na timu nzuri unashinda tu bila shida yotote. Kama kuna kitu rahisi kwa sasa kwa Yanga, basi ni kucheza na Simba. Ndiye kibonde wao. Simba imepotea njia watu wanajipigia tu. Kama Ihefu na Singida hawaogopi tena, hii ndiyo mbaya zaidi. Pale kwenye ukuta wa Simba nadhani anahitajila mtu mmoja wa kucheza na ama Henoc Inonga au CheMalone. Hawa walinzi mabeki nawaona ni kama wanafanana kila kitu. Anahitajika mtu mmoja ngumu wa kucheza nao.

Nimemuona Ayoub Lakred sio kipa mbaya lakini anahitajika  mwingine wa daraja la juu.
Kipa na mshambuliaji ni kazi ngumu kuwapata. Inahitaji utulivu na muda. Ukiitazama pia Simba kwenye kiungo unaona wanatakiwa kuja watu wengine hata wawili wa kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza. Simba imepoteza ubora wake. Siku hizi watu wanajipigia tu. Hakuna anayeiogopa tena Simba.

Kwa timu inayopigania ubingwa inahitaji kuleta wanaume wa shoka pale. Ni muda wa kuvunja mikataba ya baadhi ya wachezaji hasa wa kigeni na kuleta washambuliaji wa maana. Pale mbele kwa Simba, papatupapatu zimekuwa nyingi.

Ni muda wa kwenda kuwatafuta kina Meddie Kagere wapya. Ni muda wa kwenda kuleta watu aina ya Chris Mugalu. Ni muda wa kupata mtu kama John Bocco. Tofauti na hapo, Simba itaendelea tu kuchezewa sharubu.