TUKUTANE SAA 10 VPL

BAADA ya siku 315 za matokeo ya furaha na huzuni kwa nyakati tofauti, Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020-2021 inafikia tamati leo wakati timu zote 18 zitakapocheza mechi za mwisho leo katika viwanja tisa tofauti, huku vita kubwa ikiwa eneo la mkiani ya kuepuka kushuka daraja.
Ni mechi tisa zitakazotimiza jumla ya michezo 306 ya msimu huu ulioanza Septemba 6 mwaka jana ikiwa na maana kwa muda wa wiki 45 sawa na miezi 10 na siku 12 zaidi ya wachezaji 500 walikuwa wakizitetea timu zao katika Ligi Kuu, japo Mwadui walisalimu amri mapema.
Mwadui imekuwa timu ya kwanza kushuka daraja na kuwaachia wenzake msala wa kupambana kuepuka kuwa miongoni kwa timu tatu za kuungana kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao na nyingine kuangukia hatua ya mtoano za kucheza na Pamba na Transit Camp ili kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao au kuungana na nne zitakazoshuka mapema leo.
Tayari Simba, Yanga, Azam na Biashara United zimeshajihakikisha kuwepo katika Nne Bora na kukata tiketi ya kimataifa, lakini timu nyingine zilizosalia zikiwa kwenye vuta nikuvute za kuepuka kushuka au kuangukia hatua ya mtoano ambayo msimu uliopita iliondoka na Mbao FC ya Mwanza.
Leo inaweza kuwa siku ya majonzi na vicheko kwa baadhi ya timu kulingana na matokeo yatakayopatikana ambayo mwishoni ndio yataamua nafasi ambayo timu husika itamaliza katika msimamo wa ligi.
Kwa mujibu wa ratiba mechi za leo zitachezwa muda mmoja kuanzia saa 10:00 jioni, ambapo mabingwa Simba wataikaribisha Namungo Uwanja wa Benjamini Mkapa, huku Yanga ikiwa ugenini mjini Dodoma kuvaana na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Mechi nyingine na uwanja kwenye mabano ni kama ifuatavyo, KMC v Ihefu (Uhuru, Dar), Ruvu Shooting v Azam (Mabatini, Pwani), Mbeya City v Biashara United (Sokoine, Mbeya), Tanzania Prisons na Gwambina (Nelson Mandela, Sumbawanga), JKT Tanzania v Mtibwa Sugar (Azam Complex, Dar) Coastal Union v Kagera Sugar (Mkwakwani, Tanga), wakati Polisi Tanzania itaialika Mwadui (Ushirika, Moshi).
WANAOSHUKA
Mwadui FC tayari imeshashuka moja kwa moja daraja na leo hii itaungana na timu nyingine tatu ambazo zitamaliza katika nafasi ya 15, 16 na 17. Timu sita ndizo ziko hatarini zaidi na kila moja inapaswa kuchanga karata vyema kwa kuibuka na ushindi na kisha kuombea mabaya wapinzani wengine ili iweze kujihakikishia kubaki.
Hali ni mbaya zaidi kwa Coastal Union na pointi zake 37, JKT Tanzania yenye pointi 36, Ihefu iliyo na 35 na Gwambina yenye pointi 34.
Mtibwa Sugar yenye pointi 39 sawa na Mbeya City, kila moja inahitaji angalau sare tu ili iepuke kushuka moja kwa daraja na hivyo kubaki Ligi Kuu au kupata fursa ya kucheza mechi za mchujo.
TISA UHAKIKA
Timu tisa zina uhakika wa kusalia katika Ligi Kuu kwa matokeo yoyote ambayo kila moja itapata leo kutokana na kuwa na idadi ya pointi ambazo zimeziweka katika mahali salama.
Timu hizo ni Simba, Yanga, Azam, Biashara United, KMC, Namungo, Polisi Tanzania, Prisons na Ruvu Shooting.
UKAME HAT TRICK
Ligi inafikia tamati leo, huku kukiwa na ukame mkubwa wa hat trick, kwani hadi sasa zimefungwa mbili tu kupitia John Bocco wa Simba na Adam Adam aliyekuwa JKT Tanzania kabla ya kutimka Libya kucheza soka la kulipwa.
Kwa hali ilivyo hakuna uwezekano wa kuvunja au kuifikia rekodi ya msimu uliopita ambapo kulikuwa na ‘hat trick’ nane kwa msimu mzima.
AIBU KWA MWADUI
Mwadui FC ndio timu iliyoweka rekodi ya kinyonge ya kuwa timu iliyopoteza idadi kubwa ya michezo kwa kufungwa mabao mengi.
Timu hiyo ilifungwa mabao 6-1 na JKT Tanzania, ilifungwa mabao 5-0 na Simba kisha ikafungwa idadi kama hiyo na Yanga na kisha Coastal Union, kitu kinafanya kama leo haitakaza buti mbele ya Polisi Tanzania mjini Moshi.
Wagosi wa Kaya, nao wanamaliza ligi ikiwa imeweka rekodi ya kufunga idadi kubwa ya mabao msimu huu walipokumbana na kisago toka kwa Simba Novemba 21, 2020 kwa kufumuliwa mabao 7-0 mjini Arusha. Hakuna timu iliyofumuliwa idadi kubwa kama hiyo msimu huu.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha Msaidizi wa Gwambina, Khasain Salum alisema licha ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City, lakini matumaini yao ni kushinda mechi ya mwisho leo mbele ya Prisons.
“Lengo letu lilikuwa kushinda mechi hiyo lakini haikuwezekana, hatujakata tamaa na sasa akili na nguvu tunazielekeza kwa Prisons kuhakikisha tunashinda” alisema Salum naye Kocha wa Mbeya City, Mathias Lule alisema bado kazi haijaisha japokuwa ushindi wao wa juzi uliamsha matumaini ya wao kusalia Ligi Kuu na kwamba wataingia leo uwanjani kwa akili kuwabana Biashara United.
“Wapinzani wetu hawatakuwa na presha kwakuwa wao wameshajihakikishia kubaki Ligi Kuu, lazima niwaandae vyema nyota wangu kisaikolojia kuhakikisha tunashinda mechi hiyo” alisema.
Naye Kocha wa Prisons, Shaban Kazumba alisema wanahitaji heshima katika mechi hiyo na kwamba hawatawadharau wapinzani kwa matokeo yao waliyonayo hadi sasa.
“Mechi itakuwa ngumu kwa sababu kila timu inahitaji matokeo mazuri, sisi tunataka heshima kwahiyo lazima tujiandae kuhitimisha Ligi kwa kishindo” alisema Kazumba, huku Patrick Okumu anayeinoa Biashara alisema hawatakubali kuchafua ubao wao kwa kuruhusu alama tatu na kwamba Mbeya City wajiandae kisaikolojia kupokea kipigo.