Sven aachiwa msala Simba

Sven aachiwa msala Simba

KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck ameachiwa msala na mabosi wake juu ya kuamua hatma ya kocha wa makipa wa kuchukua nafasi ya Mharami Mohammed ‘Shilton’.

Kamati Ndogo ya Usajili ya Simba imemkabidhi kocha huyo majina ya makocha watatu wa makipa ambao walifanya usaili kati ya wengi waliomba nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Shilton aliyetimuliwa sambamba na Meneja, Patrick Rweyemamu mwezi uliopita.

Mwanaspoti iliwahi kuwadokeza kuwa miongoni mwa majina hayo matatu limo jina la Mkenya, Idd Salim ambaye aliwahi kufanya kazi katika kikosi hicho mwaka 2017, akiwanoa makipa Daniel Agyei, Peter Manyika Jr na Denis Richard, lakini Sven amegoma kuwataja majina kwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Sven alithibitisha kuwa, tayari amepitia wasifu (CV) wa makocha wote wameonekana kuwa na vigezo bora na sasa jukumu lake kupitisha jina moja tu.

Alisema baada ya kupokea CV hizo kutoka kwa viongozi alitenga muda wa kutosha kuzisoma na kuzifuatilia na kuamini ni makocha wanaostahili na wote wanaweza kwenda kufanya naye kazi ila nafasi inayohitajika ni moja tu.

“Ni vigumu kutaja majina yao kwani tupo katika hatua za mwisho ili kumpata mmoja kati yao, ila kati ya hao watatu wapo wageni na mzawa na kabla ya kumchagua mmoja kuna mambo mawili ninayotaka kufanya nao kwanza kabla ya kupitisha mmoja,” alisema Sven.

“Kwanza nataka kuonana nao ana kwa ana kila mmoja kwa wakati wake ili kuzungumza naye kile walichokiandika katika CV yake, atakachoenda kukifanya kwa makipa wetu, kwa namna gani na nitamuuliza maswali ya kujenga ili kuwa na mtu sahihi,” alisema Sven na kuongeza;

“Unajua kila mmoja anayeomba kazi lazima CV yake itakuwa imejitosheleza na kueleza mambo mengi aliyofanya huko nyuma ila mimi namtaka yule ambaye atakwenda kufanya ya wakati ujao.

“Jambo la pili nitakwenda na kila mmoja mazoezini kwa muda wake na kumkabidhi makipa wote watatu na nitamuangalia atakachokifanya kulingana na tunavyotaka kwa upungufu uliopo.

“Nitakayemchukua, ni yule atakayefiti katika falsafa zangu za kufundisha soka ili kile ambacho nitakuwa nakitoa kwa wachezaji wa ndani kiwe rahisi kuingia kwa makipa kwani tutakuwa naendana naye,” alisema Sven, aliyesisitiza kazi hiyo itafanyika kabla ya kwenda Nigeria.

“Kazi hiyo hii nitaifanya mapema kwani kabla ya kucheza mechi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika nitakuwa nimeshawakabidhi viongozi jina na watamalizana naye ili kumsajili na kuanza kazi,” aliongezea Sven aliyeipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita likiwa ni taji la la tatu mfululizo la ligi kwa klabu hiyo, mbali na Ngao ya Jamii na Kombe la ASFC.

Simba imepangwa kuanza mechi yake ya awali za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United ya Nigeria kati ya Novemba 27-29 kabla ya kurudiana nao mwezi ujao.

_________________________________________________

BY THOBIAS SEBASTIAN