Staa Yanga: Tunabeba kirahisi

STAA wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’(pichani) ameona ushindani wa ubingwa wa Ligi Kuu Bara umebakia kwa klabu kongwe Simba na Yanga, huku nyingine zikifanya kazi ya kubakia msimu ujao na kumaliza nafasi za juu. Lakini akakoleza kwamba kwa kasi Yanga wanayokwenda nayo hana wasiwasi nayo hata kidogo.

“Japokuwa Yanga inaongoza ligi kwa pointi 44 katika mechi zao 18, ikishinda 13, sare tano, wakati Simba ina pointi 35 kwa mechi 15, imeshinda 11, sare mbili na imefungwa miwili haimanishi kwamba vita yao imeishia hapo,” alisema Jembe Ulaya na aliongeza kuwa:

“Sioni juhudi za timu nyingine kupambania ubingwa, unaona zinaridhika kupigania kubakia kwenye ligi, nyingine kuishia nafasi za juu, mfano Azam FC unaona kabisa imepunguza ari ya ushindani na ndio ilikuwa inatazamwa ingekuwa inaleta chachu dhidi ya hizo kongwe,” alisema.

Alisema angalau Namungo iliyochini ya kocha Hemed Morocco anaona inaweza ikaleta ugumu dhidi ya Simba na Yanga kupata matokeo kirahisi, jambo analolifurahia kwa ajili ya afya ya soka nchini.

“Achana na kile Namungo ilikifanya Kombe la Shirikisho nakufikia hatua ya kucheza play off na timu zilizotolewa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia ina kitu chakuichangamsha ligi, Simba na Yanga zinapokwenda kucheza nazo lazima zizifikirishe,” alisema.

Straika wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella naye alisema: “Yanga kuongoza ligi haimanishi kwamba tayari imekuwa bingwa, badala yake naona vita ama mshindani wake ni mtani wa jadi Simba, lakini kwa timu nyingine unaona kabisa hazijibishi kutamani ubingwa bali na zenyewe unaona kabisa zinazitazama hizo kongwe.”

Ligi Kuu Bara msimu huu imekuwa na ushindani wa aina yake kila mmoja akipambana.