Simba: Tulieni vifaa vinakuja, Try Again atoa siri

Wednesday July 06 2022
Simba PIC
By Thobias Sebastian

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema baada ya kupoteza makombe yote msimu huu sasa wanajipanga na msimu ujao kikosi chao kitakuwa bora zaidi kulingana na usajili bora waliofanya wakati huu wa dirisha kubwa la usajili.

Try Again alisema jambo la kwanza walichukua ripoti ya kocha wao aliyeondoka, Pablo Franco pamoja na mawazo ya baadhi ya viongozi wenye uelewa wa masuala ya kiufundi kisha wakaenda sokoni kutafuta wachezaji wa maana.

Alisema msimu uliopita walisajili wachezaji wengi kwenye dirisha kubwa ila kuna wengine hawakuwa katika viwango bora lakini msimu ujao hilo halitatokea kutokana na vigezo vya kiufundi walivyozingatia.

“Yale mapungufu yaliyoonekana msimu uliopita hadi tukashindwa kufanya vizuri na kushindwa kutimiza malengo yetu hasa mashindano ya ndani msimu ujao sidhani kama tunaweza kukutana nayo,” alisema Try Again na kuongeza;

“Tumekuwa kimya katika usajili kutokana na utulivu wa kutafuta wachezaji wazuri na wenye uwezo ambao tumewafuatilia kwa muda mrefu kama Moses Phiri ili kuongeza makali msimu ujao,”

“Niwahakikishie mashabiki wetu watulie msimu ujao tutakuwa na timu nzuri kutokana na usajili wetu tuliofanya msimu huu pamoja na wale wachezaji ambao tutabaki nao kikosini.

Advertisement

“Wakati huu tunaendelea kufanya mambo mengine ya kiufundi kwa ajili ya msimu ujao ikiwemo usajili huku tukimuhusisha kocha mpya, Zoran Maki ambaye amekuwa akitoa mchango wake wa mawazo.”

Kocha mpya wa Simba, Maki, wachezaji wapya na wale waliomaliza msimu na kikosi hicho wapo kwenye mipango ya msimu ujao wanatakiwa kuwa Dar es Salaam Julai 13 kwani kati ya Julai 14 au 15 wataondoka nchini kwenda kwenye moja ya nchi iliyokuwa na asili ya Kiarabu Afrika kwa ajili ya kambi (Pre season). Mwanaspoti linajua Simba inaenda kambini Misri.

Nyota waliosajili lakini hawajawatangaza ni Vicent Akpan, Augustine Okra, Habibu Kyombo, Ceasar Lobi Manzoki, Nassoro Kapama na Phiri ambaye ametangazwa tayari wiki kadhaa nyuma.

Advertisement