Simba kuoga minoti kwa Orlando

Sunday April 24 2022
Simba PIC
By Mwandishi Wetu

SIMBA kesho Jumapili wana kazi moja tu ya kuhakikisha wanaiondoa Orlando Pirates kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika iwe kwa sare yoyote au ushindi.

Hiyo ni baada ya awali kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam walipowafunga wapinzani wao hao bao 1-0 ikiwa ni mechi ya kwanza ya hatua ya robo fainali ambapo kesho wanacheza mechi ya marudiano.

Haijalishi Orlando Pirates kujipanga wakiwa nyumbani lakini Simba chini ya kocha wao Pablo Franco wamejipanga kusonga nusu fainali ambayo licha ya kupiga hatua kubwa lakini watajizolea pesa nono kutoka CAF.

Matokeo yoyote mazuri yatakuwa na neema kwa nyota wa Simba kwani watavuna kiasi kikubwa cha fedha za bonasi waliozoahidiwa na uongozi wao.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti linazo ni kuwa miongoni mwa ahadi ambayo wameahidiwa ni kupewa zaidi ya asilimia 75 ya fedha za zawadi ambazo watazipata kutoka CAF kwa kutinga nusu fainali ambayo kila timu inayoingia inavuna kiasi cha Dola 450,000 (Sh1 bilioni).

Asilimia 75 ya Sh 1 bilioni ni takribani Sh750 milioni ambazo kama zikigawanywa kwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la timu hiyo, kila mmoja ataweka mfukoni kiasi Sh18.7 milioni.

Advertisement

Kikosi cha Simba kinaundwa na takribani watu 40 ambao ni wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi ambao kiasi hicho cha sh 750 milioni watakachopata kikigawanywa kwa idadi yao, kama wakigawana pasipo kuangalia ushiriki wa kila mmoja kikosini, akaunti ya kila mtu itaondoka na Sh 18.7 milioni.

Hata hivyo, mara kwa mara mgawo wa fedha za bonasi huzingatia mchango wa kila mmoja kikosini ambapo wale wanaocheza hupata mkubwa kulinganisha na wanaotazama mechi jukwaani.

Tayari kikosi cha Simba kilitua jana nchini humo huku mtendaji mkuu Barbara Gonzalez akisema: “Tunafahamu mechi itakuwa ngumu kutokana na wapinzani wetu walivyojipanga, tunawaheshimu wapinzani lakini hata sisi tumejipanga na lengo letu ni ushindi, tunaamini tutapata matokeo mazuri.”

Kwa upande wake, Pablo alisema: “Ni mechi ngumu na tumekuwa hatuna historia nzuri ugenini lakini jambo la muhimu kukabiliana na hilo ni kujiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huu ambao tutakuwa ugenini. Orlando Pirates ni timu nzuri na wachezaji wangu wanapaswa kufanya kazi ya ziada ili tuweze kusonga mbele.”


ORLADO PRESHA

Habari zilizolifikia Mwanaspoti kutoka Afrika Kusini jana jioni zilisema mashabiki wa Orlando Pirates wamekuwa wakiizungumzia Simba kila mara na kinachowatisha ni namna ilivyoweza kuwadhibiti wachezaji wao katika mchezo wa kwanza uliopigwa Kwa Mkapa.

Kwa mujibu wa habari hizo, licha ya mashabiki mitaani kuzungumzia mchezo huo na namna kikosi cha Simba kinavyotisha, pia redio mbalimbali katika kitongoji cha Soweto zimekuwa ziijadili Simba katika vipindi vyao vya michezo, ambapo watangazaji na wachambuzi wanaitaja kuwa moja ya timu kali barani Afrika inayoweza kuwaduwaza nyumbani kwao.

Kinachozungumziwa zaidi ni namna mastaa wa Orlando walivyodhibitiwa katika mchezo uliopita, licha ya kwamba lengo ililotoka nalo nyumbani kuja Dar lilikuwa la kufunguka uwanjani ili kupata ushindi mkubwa - tena wa mapema.


Advertisement