Kapombe, Bwalya wapewa kazi spesho

Kapombe, Bwalya wapewa kazi spesho

KIKOSI cha Simba kinapaa asubuhi ya leo kwenda Afrika Kusini ili kuwahi mechi ya marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, lakini kambini kocha Pablo Franco ameamua kuwapa kazi maalumu nyota wake wawili.

Kocha huyo kutoka Hispania aliyeiongoza Simba kufikia ilipo, katika mazoezi yao ya jana asubuhi kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju alionekana akiwapa kazi maalumu beki Shomary Kapombe na kiungo Rally Bwalya.

Ili kuhakikisha Simba inatumia kila nafasi itakayoipata katika mechi hiyo ya Jumapili mjini Johannesburg, Pablo aliwapa kazi ya kupiga mipira ya frii-kiki na penalti, kama njia ya kuwatengeneza mapema kwenda kuimaliza Orlando kwao.

Kapombe na Bwalya nje ya mazoezi ya pamoja na wenzao, walipewa programu ya kupiga frii-kiki, kona na penalti kwa zaidi ya dakika 15.

Wawili hao walipiga penalti zaidi ya tano na zote kufunga na baadaye wakahamia katika frii-kiki ambapo pia Bwalya alifunga na kuongezewa Erasto Nyoni, Israel Mwenda na Pascal Wawa ambao nao walifunga.

Baada ya hapo walihamia kwenye kupiga kona kazi kazi iliyofanywa na Bwalya na Kapombe chini ya usimamizi mkubwa wa Pablo na muda mwingi walipiga kona ndefu ambazo zilichezwa na wachezaji wengine waliokuwa ndani ya boksi.

Aidha, katika nafasi nyingine, Pablo na msaidizi wake, Seleman Matola walichagua timu mbili na kuanza kucheza kama mechi na muda mwingi kuonekana wakielekeza mifumo tofauti.

Katika mifumo hiyo, makocha hao walikomaa zaidi kwenye kuelekeza mbinu za kujilinda kwa kuwataka mabeki kuwa na mawasiliano sahihi pia kukaba kwa nafasi na ustadi mkubwa.

Huenda kwenye mechi ya keshokutwa, Simba ikawaanzisha mabeki watano kwa nia ya kujilinda zaidi kutokana na namna Pablo na Matola walivyokuwa wakipanga na kusimamia mazoezi ya jana, ingawa Mhispania huyo huwa hatabiriki kirahisi.

Katika moja ya timu alizopanga ilijaa nyota wa kikosi cha kwanza, pia walipanga mabeki wa pembeni wawili na wa kati watatu kuonyesha huenda Johannesburg Simba ikaenda kulinda ushindi wao wa bao 1-0 ilioupata jijini Dar.

Mabeki waliopangwa ni Mohammed Hussein, Shomari Kapombe, Joash Onyango, Pascal Wawa na Henoc Inonga huku langoni akiwepo Aishi Manula, eneo la kiungo walinzishwa Sadio Kanoute, Jonas Mkude na Rally Bwalya, wakati mbele kulikuwa na Chriss Mugalu na Pape Ousmane Sakho.

Wachezaji wengine waliokuwepo mazoezi ni; Beno Kakolanya, Ally Salim, Ahmed Feruzi, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Taddeo Lwanga, Mzamiru Yassin, Yusuph Mhilu, Peter Banda, Meddie Kagere na Kibu Denis, huku Clatous Chama, John Bocco, Benard Morrison na Jimmyson Mwanuke hawakuonekana.