Simba akili kubwa, kocha Mfaransa ashtua

MASTAA wa zamani wa soka la Tanzania, wamefurahia akili ya Simba la kuanzisha Super Cup na kusisitiza hilo ni kama zali kwao kwani itawasaidia kujua ubora wa wapinzani wao.

Kama hiyo haitoshi habari ya kujiuzulu ghafla kwa Kocha wa El Merreikh, Mfaransa Didier Gomes imewashtua waarabu hao kwani hawakutarajia huku wakiwa na presha zaidi huenda akatambulishwa na Simba leo, jijini Dar es Salaam.

Gomes mwenye rekodi nzuri kimatokeo ndiye aliyeitoa Enyimba kwao na kutinga hatua ya makundi Afrika alikokuwa anakwenda kukwaana na Simba.

Kwa mujibu wa mitandao ya Sudan, Merreikh wamepagawa kwani hawakutarajia kujiuzulu ghafla kwa Gomes aliyeamua kulipia mkataba wake, huku wakiwaza uamuzi wa Simba kuwaita Al Hilal ambao ni wapinzani wao Dar na watacheza nao Jumatano.

Pia wanajua Simba ikimalizana nae na kumtambulisha leo itakuwa ni pigo kwani anawajua nje ndani na wanahofu kupoteza pointi sita za wakikutana.

Licha ya Simba kufanya siri kubwa, lakini Gomes mpaka jana usiku alikuwa akitajwa kama ndiye kocha mkuu wa Simba na anakuja na msaidizi wake mmoja atakayejumuishwa na mzawa Seleman Matola na Mbrazili wa makipa, Milton Nienov.

Mbali na Al Hilal, Simba imewaalika TP Mazembe ambao ni wakali wa AS Vita ambao wamepangwa kundi moja na Mnyama Afrika.

Beki wa kati wa zamani wa Simba, William Martin aliunga mkono aliyeanzisha wazo la mashindano hayo,

“Japo mifumo ya TP Mazembe na AS Vita inaweza kuwa tofauti, lakini kuna vitu vitafanana katika ligi yao, ukiachana na hilo Mazembe ni klabu kubwa yenye uzoefu na mashindano hayo, hivyo ni sahihi Simba kujipima ubavu nao,” alisema.

Mchezaji wa zamani wa Pan Africans na Yanga, Godian Mapango alisema;

“Wameonyesha soka linavyotakiwa kuwa tafu nchini. Simba inastahili kucheza na TP Mazembe na Al Hilal zenye viwango vya juu na zinazofanya vizuri Ligi ya Mabingwa, hivyo wachezaji watapata uzoefu mkubwa.”

Naye baba wa Samatta, Ally Pazi Samatta alisema; “Simba ilipofikia inastahili kucheza na timu hizo kwani zimefanya vitu vikubwa Ligi ya Mabingwa, kikubwa wachezaji wajifunze kwa wenzao ili wawe levo za juu.”


FAIDA YAKE

Faida kubwa itakazopata Simba kupitia mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Jumatano, Februari 27, Dar es Salaam yakishirikisha timu tatu ni kuongeza mapato, kujenga mahusiano bora na klabu nyingine na kunufaika kiufundi pindi yatakapomalizika.

Makusanyo ya viingilio na fungu itakalolipata Simba kutokana na kuuza haki za matangazo za mechi hizo yataisadia kupata fedha zitakazoendesha klabu katika kipindi hiki cha mtikisiko wa kiuchumi kwenye soka na michezo mingine kutokana na Corona.

Simba imetangaza kiingilio cha chini ni Sh3,000, ikiwa wataingia mashabiki 60,000 Uwanja wa Benjamin Mkapa, hii ina maana itakuwa na uhakika wa kuingiza takribani Sh180 milioni kwa mchezo mmoja na inaweza kuongezeka kutokana na uwepo wa viwango vya juu kutokana na majukwaa na ndani ya siku tano za michuano hiyo, inaweza kuingiza zaidi ya Sh500 milioni na zaidi.

Faida ya pili ni kujenga mahusiano bora na timu hizo zilizoizidi kimafanikio ndani na nje ya uwanja, kwa kubadilishana uzoefu utakaokuwa msaada kwao kupiga hatua kiutawala na uendeshaji na masuala ya kiufundi. Pia kufungua milango ya kuuza au kununua wachezaji kutoka klabu hizo.

Kukumbana na timu hizo inaweza kupata taswira ya aina gani ya ushindani itakutana nao hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika hatua ya makundi, Simba imepangwa na Al Ahly ya Misri, AS Vita Club (DR Congo) na El Merrikh ya Sudan.

TP Mazembe ndio washindani wakuu wa AS Vita katika ligi ya DR Congo na aina ya soka lao imekuwa haitofautiani sana kama ilivyo kwa Al Hilal ambao ni watani wa jadi wa El Merrikh na wanatoka katika jiji moja huku wakitumia uwanja mmoja wa Omdurman kama ilivyo wa Yanga na Simba zinazotumia Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Ukiondoa hilo, itakuwa ni fursa pia kwa wachezaji wa Simba kupata uzoefu wa ushindani dhidi ya klabu kubwa lakini pia kutoa nafasi kwa benchi jipya la ufundi la timu hiyo kufahamu uimara na udhaifu wa timu yao ili waweze kufanyia kazi kabla ya hatua ya makundi inayotarajiwa kuanza Februari 12.

Uanzishwaji wa mashindano hayo umeonekana kuwakosha wadau wengi wa mpira wa miguu ambao wanaamini yataleta tija.