Samata aiokoa KMC ikiambulia sare kwa Mbeya City

Saturday November 27 2021
Samatta PIC
By Saddam Sadick

Mbeya. Mbeya City imeendelea kuweka rekodi ya kufikisha mechi saba bila kupoteza baada ya leo kutoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC.

Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Sokoine Mbeya kila timu ilionesha ukomavu wake kwa kusaka ushindi lakini hadi kipyenga cha mwamuzi Emanuel Mwandembwa kutoka Arusha kupulizwa hakuna aliyeweza kuondoka na alama tatu.

Huo unakuwa mchezo wa saba kwa Mbeya City kucheza msimu huu bila kupoteza na kuendelea kubaki nafasi ya tatu kwa pointi 11 huku KMC wakifikisha alama sita.

Mbeya City ndio walianza kuliona lango la wapinzani dakika ya nne kupitia kwa Paul Nonga aliyemalizia pasi ya Azizi Andabwile kisha KMC kusawazisha kupitia kwa Matheo Anthony dakika ya 18 na kufanya dakika 45 za awali kwenda kwa sare hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa kila timu kufanya mabadiliko ya kadhaa, ambapo Mbeya City waliweza kuongeza bao lililofungwa na Richardson Ng'ondya dakika ya 66 kabla ya wapinzani kusawazisha dakika ya 86 kupitia kwa Mohamed Samata.

Hata hivyo dakika ya 83 mshambuliaji wa KMC, Emanuel Mvuyekule alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kugongana na Aidan Rasmos na kutolewa uwanjani kwa gari la kubebea wagonjwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Advertisement
Advertisement