Sababu ya Tarimba kujichomoa TFF

MBUNGE wa Kinondoni, Tarimba Abbas amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku akifunguka sababu ya kutorejesha fomu siku ya mwisho ya kuchukua na kurudisha fomu za uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 7.
Tarimba aliyekuwa miongoni mwa waliochukua fomu ya kuwania urais wa TFF, unaoshikiliwa kwa sasa na Wallace Karia na mpaka zoezi hilo likifungwa juzi saa 10 jioni, hakuonekana viunga vya TFF na alipotafutwa kwa njia ya simu muda mfupi baada ya zoezi kufungwa, Tarimba alisema hawezi kujiingiza kwenye fitina za uchaguzi huo.
Hata hivyo, alikataa kutaja sababu hasa za kutorejesha fomu hiyo ambayo gharama yake ni Sh500,000 akisisitiza hayuko tayari kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Tarimba alichukuliwa fomu na Dominic Salamba aliyetinga jana TFF na kurejesha fomu ya mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Ally Mayay huku akibainisha kutofahamu ya Tarimba itarejeshwa vipi japo alimchukulia.
Mpaka juzi shughuli inafungwa kwenye ugombea urais waliorudisha fomu walikuwa sita kati ya 10 waliochukua juzi ambao ni, Ally Mayay, Ally Saleh, Hawa Mniga, Oscar Oscar, Wallace Karia na Evans Mgeusa.
Mbali ya Tarimba walioshindwa kurejesha ni pamoja na Deogratius Mutungi, Rahim Kangezi na Zahor Mohammed Haji.
Kwenye nafasi ya ujumbe waliorejesha fomu ni 26 kutoka kanda sita tofauti na sasa wanasubiri kufanyiwa usaili na taratibu nyingine ili kupitishwa kwenda kupigiwa kura jijini Tanga.