Rekodi zaibeba kiutamu Simba

HAWACHOMOKI. Ndivyo unavyoweza kusema kutoka na rekodi tamu iliyonayo Simba kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya timu za Afrika Kaskazini kabla ya kesho kuvaana na RS Berkane ya Morocco.
Rekodi hizo nzuri za Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya timu za ukanda wa Kaskazini maarufu kama Waarabu zinaibeba Simba katika mechi yao ya kesho ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tangu 1974 ilipoinyoosha Mehala El Kubra ya Misri katika hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), Simba imekuwa na rekodi nzuri kwa timu hizo za Kaskazini, kiasi cha nyota wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa kusema Wekundu hao washindwe wenyewe tu kesho.
Pawasa anaamini kwa rekodi zilivyo, Uwanja wa Mkapa utaendelea kuwa machinjio kwa Berkane katika mechi hiyo ya Kundi D itakayochezwa kesho kuanza saa 10:00 jioni.
“Waarabu wamekuwa wakitusumbua kwao lakini si hapa, tumekuwa na rekodi nzuri dhidi ya timu za ukanda huo, sio kwa miaka ya hivi karibuni tu, hii ni tangu na tangu, na sidhani kama rekodi hiyo inaweza kuvunjwa,” alisema Pawasa.
“Kikubwa ni kucheza kwa nidhamu, haya mambo ya rekodi si vizuri kuwa vichwani mwa wachezaji na kusahau kutekeleza majukumu yao ya msingi,” aliongezabeki huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania.
Rekodi zinaonyesha Februari 23, mwaka jana ndio ilikuwa mara ya mwisho kwa timu za Kaskazini kuja nchini na kutandikwa ambao ndio watetezi wa Ligi ya Mabingwa, Al Ahly ya Misri.
Al Ahly ikitoka kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa Klabu na kumaliza ya tatu, ilishindwa kuhimili vishindo vya Simba kwa kucharazwa bao 1-0 kupitia Luis Miquissone msimu huu na kuendeleza moto wake kama kawaida huko.
Timu nyingine zilizoshindwa kutamba mbele ya Simba ikicheza nyumbani ni Al Ahly hao hao waliobamizwa mabao 2-1 jijini Mwanza mwaka 1985, kisha kuchapwa tena 1-0 mwaka 2019.
Arab Contractor inayojulikana kwa sasa kama Mokawloon ikachapwa 3-0 mwaka 1996, Ismailia ilifungwa bao 1-0 mwaka 2001 na mwaka 2003 Ismailia ikalazimisha suluhu na Zamalek ikafa bao 1-0 mwaka 2003 kabla ya kwenda kuvuliwa taji la Ligi ya Mabingwa kwa penalti na Wekundu wa Msimbazi hao.
Mwaka 2010, Simba iliiadhibu El Hahoud mabao 2-1, na ikatoka sare 2-2 dhidi ya Al Masry mwaka 2018.
Timu za Waarabu kutoka nje ya Misri ni USM Al Harach ya Algeria iliyofungwa mabao 3-0 mwaka 1993, ES Setif mwaka 2012, iliyofungwa 2-0 na JS Soura aliyotua nchini ikiwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Kitanzania, Thomas Ulimwengu na kuchezea bakora 2-0.