Prisons, City derby ya rekodi na visasi

Muktasari:
- Rekodi inaonesha msimu huu Mbeya City haijapoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu kwenye uwanja wa Sokoine, huku Prisons ikipoteza michezo miwili tangu ianze kutumia uwanja huo na kesho inasaka ushindi wa kwanza na kufuta uteja kwa wapinzani.
Mbeya. Baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo katika uwanja wa Sokoine, Tanzania Prisons imesema kesho Jumapili haitarajii kurudia makosa kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya ndugu zao, Mbeya City na kujinasua nafasi za mkiani.
Maafande hao ndio watakuwa wenyeji katika mchezo huo ukiwa wa tatu tangu warejee kwenye uwanja huo wakitokea mkoani Rukwa ambapo mambo hayakuwa mazuri huku wakiwa hawajapata ushindi kwani mechi mbili walizocheza jijini Mbeya wamepoteza zote ikiwa ni dhidi ya Polisi Tanzania mabao 2-0 katika mchezo wa kombe la shirikisho na Ruvu Shooting iliyowatandika bao 1-0.
Mchezo baina ya timu hizo unavuta hisia kubwa kwani kila timu inahitaji ushindi japokuwa Mbeya City inawakabili wapinzani hao ikiwa na kumbukumbu ya ushindi kwenye mchezo wa raundi ya kwanza walipoilaza bao 1-0 hivyo kufanya mpambano huo kuwa wa rekodi na visasi.
Kocha Msaidizi wa Prisons, Shaban Kazumba amesema pamoja na ugumu wa mechi hiyo kutokana na timu zote kujuana lakini wamejipanga kushinda na kujinasua nafasi za chini huku akieleza kuwa vijana wake wako fiti na tayari kwa mpambano.
"Tunajua ugumu wa mchezo kwani tunapokutana na Mbeya City huwa mechi inakuwa na ushindani tunawajua wanatujua, hivyo makosa tuliyoyafanya katika mechi iliyopita tumeyarekebisha hivyo kesho ni ushindi" amesema Kazumba.
Naye nyota wa timu hiyo, Salum Upuu amesema hawawezi kulinganisha mchezo wa 'Derby' na matokeo yaliyopita, isipokuwa wanaenda kupambana kuhakikisha wanapata ushindi na kwamba wachezaji wote hakuna anayefurahia matokeo waliyonayo kwa sasa.
"Kesho ndio tunaenda kuanza Ligi, haya matokeo siyo mazuri na hakuna mchezaji anayafurahia ukizingatia heshima tuliyonayo hapa Mbeya hivyo kuanzia kesho mashabiki wataona mabadiliko" amesema Upuu.
Nahodha Msaidizi wa Mbeya City, Paul Nonga amesema licha ya wapinzani kutokuwa na matokeo ya kuridhisha lakini wanawaheshimu kwani wana kikosi bora hivyo wanaenda kupambana kupata ushindi na kupanda nafasi za juu.
"Mashabiki waje kwa wingi wachezaji tumejipanga kushinda mchezo huo ili kupanda zaidi nafasi za juu, Prisons tunawaheshimu sana japokuwa hapo nyuma wamekuwa na matokeo yasiyoridhisha, tunawaahidi furaha kesho" amesema Nonga.
Naye Kocha wa Makipa wa City, Ally Mustafa 'Baltez' amesema mchezo huo utakuwa mgumu na atakayejianda vizuri ndani ya dakika 90 ndiye ataondoka na alama tatu, huku akisisitiza kuwa matarajio yao ni kushinda kwani mechi ya mwisho walipoteza ugenini dhidi ya Namungo.
"Kila timu inahitaji ushindi ili kujiweka pazuri lakini niseme Mbeya City tumejipanga zaidi na mechi itakuwa ngumu, hivyo atakayekuwa amejianda zaidi atapata pointi tatu" amesema Bartez.