Pluijm: Ile Yanga yangu ilikuwa kisu!

ILE ilikuwa Yanga buana. Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm amejitamba akiwa kwake Ghana kwa kusema kikosi ambacho alikisuka msimu ambao walitinga hatua ya makundi katika kombe la Shirikisho Afrika (2016) hakijawahi kutokea tangu aachane na timu hiyo.
Hans ambaye aliachana na Yanga mwaka 2017 huku nafasi yake ya ukocha ikichukuliwa na George Lwandamina, alisema kikosi kile kimekuwa kikimjia kichwani mara kwa mara maana alikuwa akipata tabu kufanya uchaguzi.
Kocha huyo (71), alisema; “Sikuwa na kazi kubwa ya kufanya kwa sababu nilikuwa na wachezaji wenye kushika kwa haraka maelekezo. Nilikuwa na Niyonzima, Kamusoko kati kati walikuwa wakicheza kwa spindi na kupiga pasi nyingi za mbele,” alisema.
“Kuna muda ilibidi wacheze wote, Tambwe na Ngoma kwa sababu nilikuwa nikipata tabu kufanya uchaguzi, kila mmoja alikuwa na soka lake tofauti na walijua kufunga, mmoja alikuwa akiumia sikuwa na hofu ya kubaki na mshambuliaji mmoja kwa sababu waliliokuwa wakicheza pembeni nao waliweza kufunga.”
Pluijm aliisaidia timu hiyo kubeba mataji mawili ya Ligi Kuu Tanzania Bara (Vpl), Ngao za hisani mara mbili na Kombe la FA mara moja.
Mwaka 2016, Hans aliamini walikuwa na uwezo wa kufika hata hatua ya nusu fainali ambayo viongozi wa Yanga yalikuwa matamanio yao baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika Ligi na michezo ya awali hadi kutinga hatua hiyo.
“Kilikuwa kipindi chetu lakini uzoefu ulituangusha tulipambana lakini pointi tulizopata hazikutosha kuvuka hatua ya makundi na kwenda nusu fainali.”
Yanga ambao walimaliza wakiburuza mkia walipangwa kundi moja A na klabu nyingine ambazo ni TP Mazembe ya DR Congo, Mo Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.
Katika hatua hiyo ya makundi Yanga walishinda mechi moja dhidi ya Mo Bejaia kwa bao 1-0 (Kamusoko), wakatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Medeama (Msuva) zote zilikuwa nyumbani, wakapoteza michezo minne.
JESHI LA PLUIJM 2016
Kikosi hicho, Makipa, Deo Munishi na Benno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Andrew Vincent, Mbuyu Twite, Oscar Joshua na Juma Abdul. Waliobaki hapo hadi leo ni Dante na Abdul ambaye ni nahodha wa Yanga.
Viungo na washambuliaji, Juma Makapu, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Deus Kaseke, Haruna Niyonzima na Donald Ngoma. Waliobaki ni Niyonzima, Kaseke waliondoka na kurejea, Makapu ambaye kwa sasa anachezwa beki.