Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pira la Sure Boy lamdatisha Nabi

ACHANA na Said ‘Saido’ Ntibazonkiza na kazi kubwa anayoifanya ndani ya kikosi cha Yanga akifunga na kutengeneza mabao yaliyoiweka timu hiyo kileleni mwa msimamo, unaambiwa pira tamu la kusuuza roho linalopigwa na kiungo mwingine fundi ndani ya kikosi hicho, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ limempagawisha Kocha Nasreddine Nabi aliyefungua kinywa chake na kutamka ‘huyu jamaa ubora wake sio wa nchi hii kabisa’.

Sure Boy ameanza katika mechi mbili zilizopita za Yanga na kikosi hicho kikishinda lakini ubora wake akiwa katikati ya uwanja ndio umemshtua kocha Nabi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema hana shida na ubora wa Saido, lakini ameshtushwa na ubora wa Sure Boy akiwa katikati ya uwanja akikiri kwamba hakuwahi kuona mtu bora kama huyo raia wa Tanzania tangu atue nchini.

Nabi alikiri kwamba mpaka anapitisha usajili wa kiungo huyo hakuwa anamjua kwa kina juu ya ubora wake kama huo lakini sasa nafsi yake imekubali kwamba kiungo huyo ni moto kwelikweli.

“Kusema ukweli sikuwa namjua Sure Boy kabla, sikuwahi kumuona sana uwanjani lakini kutokana na mikanda michache na sifa nilizopata nilikubaliana na wenzangu, sasa nimejua ubora wake na kusema ukweli nimeshtuka,” alisema Nabi.

“Huyu ni kiungo aliyekamilika na alizaliwa kucheza katikati ya uwanja hasa kiungo wa juu mchezeshaji, mambo anayoyafanya ni ya akili kubwa sana, sijaona mtu bora kama huyu katika ligi ya hapa Tanzania tangu nifike.”

Nabi aliongeza kwamba kati ya mambo ambayo ameyaona bora kwa kiungo huyo ambaye ni mtoto wa staa wa zamani wa Yanga, Abubakar Salum ni juu ya ubora wa pasi zake za kwenda mbele na jinsi anavyojua kuwapa shida wapinzani kupitia mikimbio yake.

Alisema kwa ubora ambao Sure Boy ameonyesha katika mechi hizi mbili kama ataendelea hivyo kikosi chake kitakuwa na silaha nyingine mpya ambayo itawapa gia kubwa ya kuusaka ubingwa.

“Anajua sana kutoa pasi (Sure Boy) pasi zake nyingi zina madhara sana hata wanapopambana kumzuia bado inakuwa shida, lakini kitu bora zaidi ni jinsi anavyofanya hesabu zake na mikimbio yake, huyu ni mmoja kati ya watu bora ambao tunao wenye ubora wa kucheza katikati ya uwanja,” alisema Nabi na kuongeza;

“Kinachotakiwa sasa ni kuendelea kucheza kwa ubora huu au zaidi, unajua kama atafanya hivi zaidi tutakuwa ni kama tumepata gia mpya ya kuzidi kuutafuta ubingwa, nimeambiwa sasa anaichezea klabu ambayo anaipenda katika maisha yake hili ni kubwa zaidi hapa kwetu.

“Unakuwa na Sure Boy, Saido, Aucho (Khalid), Feisal (Salum), Mauya (Zawadi) na Bangala (Yannick) hapo unakamilisha kundi bora la viungo wa kazi katika timu yako ambao watakufanyia kazi nzuri.”

Yanga inaondoka leo jijini Dar kwenda Mwanza kuwahi mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, huku ikiwa ipo kileleni mwa msimamo ikikusanya pointi 42 kupitia mechi 16 na kufunga mabao 28 na yenyewe wavu wake ukiguswa mara nne.

Straika raia wa DR Congo, Fiston Mayele ndiye kinara wa mabao wa Yanga akifunga tisa akifuatiwa na Saido mwenye mabao sita, huku Feisal Toto akitupia manne na Aucho amefunga matatu hadi sasa akilingana na winga Jesus Moloko.