Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pablo apata dawa mpya Simba

Kilichomtibua Pablo ni hiki, aomba radhi

KIKOSI kamili cha Simba kinatarajiwa kusepa jijini Dar es Salaam leo kwenda Zanzibar kwa ajili ya kuwasha moto kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2022, huku kocha mkuu wake, Pablo Franco akisema ameipata dawa na mikwaju ya penalti.

Simba juzi kwenye pambano lao la Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam, ilipoteza penalti kupitia kiungo fundi wao kutoka Zambia, Rally Bwalya, ikiwa ni mkwaju wao wa nne msimu huu kupoteza kwenye mechi mbalimbali za kimashindano.

Bwalya alipoteza mkwaju huo baada ya kipa wa Azam Hussein Salula kuudaka, ingawa marudio ya televisheni ya Azam yalionyesha kama kipa huyo alitoka mapema kabla ya Bwalya hajapiga na ilipaswa penalti hiyo kurudiwa.

Hata hivyo, kocha Pablo aliwatuliza wanasimba kwa kuwaambia tayari ameipata dawa ya kupoteza penalti wanazopata kwenye michezo, akiahidi jambo hilo halitajirudia tena kuanzia sasa, wakienda Zanzibar kwenye Mapinduzi ambako ishu za penalti ni kawaida sana.

Michuano ya Mapinduzi inaanza kwenye hatua ya makundi na timu zinazosonga mbele hucheza mtoano ambapo ni aghalabu kuwepo kwa hatua ya kupigiana penalti, kitu ambacho Pablo ni kama amejishtukia na kuanza kujipanga mapema. Msimu uliopita wa michuano hiyo, Simba ilipasuka katika fainali mbele ya Yanga kwa mikwaju ya penalti.

Simba ilipoteza penalti yao ya kwanza msimu huu katika Ligi ilipovaana na Biashara United mjini Musoma, pale nahodha wake, John Bocco aliposhindwa kuifunga mbele ya kipa James Ssetuba aliyeipangua na kufanya pambano hilo kumalizika kwa suluhu.

Wekundu hao walipoteza tena penalti nyingine kwenye mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting baada ya mkongwe, Erasto Nyoni kushindwa kumtungua kipa Mohammed Makaka aliyeiokoa katika mchezo ulioisha kwa Simba kushinda mabao 3-1.

Winga Mghana, Bernard Morrison naye alikosa penalti katika pambano la mtoano la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia, licha ya Wekundu hao kushinda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kusonga mbele kuingia makundi.

Ndipo juzi tena mbele ya Azam, Bwalya akaikosesha mkwaju huo, ingawa Simba ilishinda maao 2-1. Kabla ya kukosa mkwaju huo, Bwalya aliwahi kuifungia Simba penalti katika pambano dhidi ya Polisi Tanzania na kuipa ushindi mwembamba wa bao 1-0.

Mwanaspoti lilimtafuta Pablo kutaka azungumze juu ya mwenendo wa wachezaji wake kupoteza penalti, licha ya kuwa klabu iliyopewa penalti nyingi (4) hadi sasa katika ligi ikifuatiwa na Mtibwa Sugar yenye tatu, ambao wamefunga mbili na kupoteza moja.

Pablo alisema anaenda kulifanyia kazi tatizo hilo na kwamba tayari ameshajua shida ilipo kwa wachezaji wanaopata nafasi ya kupiga adhabu hiyo kwa timu yake.

“Ni kweli kuna changamoto kwenye upigaji wa penalti alikosa Bocco, Erasto na Bernard Morrison na leo (juzi) Bwalya. Uzuri bado nina muda mfupi kikosini tutaendelea kurekebisha. Tatizo ni kukosa kujiamini tu,” alisema Pablo na kuongeza;

“Upigaji wakati mwingine ni kushindwa kukaa vizuri wakati wa upigaji, naenda kuwajengea hali ya kujiamini ili inapotokea wasirudie tena makosa, japo kukosa penalti kwa mchezaji sio kitu cha ajabu, kwani haina uhakika wa 100 kwa 100 kufunga, kama kipa ni nzuri na anayejua kumsoma mpigaji.”

Pablo alisema bado hana muda mrefu ndani ya timu na kuna mambo anaendelea kuyarekebisha taratibu ili timu iwe imara wakati huu ikienda kwenye Mapinduzi na ikiwa na kibarua cha michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwenye Shirikisho Afrika, Simba imepangwa Kundi D na timu za RS Berkane ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na US Gendarmarie ya Niger na itaanza mechi yake ya kwanza nyumbani Februari 13 dhidi ya Asec kabla ya kuzifuata USGN na Berkane ugenini.