Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

OSCAR JOSHUA Yanga hii ni zaidi ya balaa!

WALIOSEMA Simba mwenda pole ndiye mla nyama wala hawakukosea, kwani beki wa zamani wa kimataifa wa Yanga, Oscar Joshua ‘OJ’, anachokifanya nje ya uwanja kinaonyesha ni jinsi gani anafurahia maisha kwa raha zake.

Joshua aliachana na Yanga mwaka 2017 na kuwa kimya akifanya yake, kabla ya Mwanaspoti kuamua kumsaka na kufanya mahojiano maalum baada ya kuwa kimya na mashabiki kuhoji yupo wapi na anafanya nini, naye akaamua kufichua jinsi anavyopambana kuifukuzia shilingi nje ya uwanja kwa sasa.

Beki huyo wa kushoto aliyekuwa na mwili jumba amefichua mambo mengi ikiwamo maisha yake ndani ya Yanga na kile ambacho kwa sasa anakifanya na kuzungumzia changamoto ambazo hawezi kuzisahau katika soka kipindi akicheza.

Pia beki huyo anakiri Yanga enzi za Yusuf Manji ilikuwa ni zaidi ya balaa na kusema itachukua muda mrefu kupata skwadi tamu kama lile, lililowatoa nishai mpaka Al Ahly baada ya uteja wa miaka zaidi ya 30 ya kupigwa nje ndani tena kwa idadi ya mabao ya fedheha. Tiririka naye...!

AJITOSA KWENYE BIASHARA

Joshua anasema baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga mwaka 2017, aliamua kujikita kwenye shughuli za biashara kwa kufungua duka la kuuza simu, camera, laptop na vifaa vingine mbalimbali vya kisasa vya umeme.

Hata hivyo, anabainisha kuwa biashara aliianza mapema kuifanya tangu wakati akikipiga Toto Africans ya Mwanza aliyoichezea kwa misimu mitatu ya 2006-2008, ambapo alikuwa ananunua kila toleo jipya la simu mpya dukani, alikuwa anatumia na kuuza kwa wachezaji wenzake.

Baada ya kujiunga na Yanga aliendeleza biashara hiyo kwa kujiweka karibu na wafanyabiashara wa simu wa Kariakoo, ili kujua aanzie wapi, lakini kwa kuwa alikuwa na nia ya kufika mbali.

“Baada ya kuwaambia wafanyabiashara kwamba nina wazo hili, wakanishauri nifanye biashara hiyo. Nikaanza kwa kushirikiana nao, tukapata fremu na kuagiza mzigo kisha nikaanza,” anasema.

“Akili yangu ilikuwa inawaza kuna maisha baada ya soka, hivyo nilianza kujipambanua mapema.Kuna wakati nilikuwa nawakopesha wachezaji pesa nikiwa Yanga na baada ya muda walikuwa wananirudishia,” anasema Joshua bila kuainisha mtaji alioanza nao katika biashara hiyo iliyokuwa kwa sasa akifuata mzigo nje ya nchi tofauti na ilivyokuwa zamani.

Anasema mzigo wa biashara zake anafuata Afrika Kusini, Dubai na Misri na kusisitiza; “Vitu vyangu sio feki kwa sababu natunza jina langu, lakini pia nauza na vifaa vya michezo.”

KWENYE KILIMO YUPO

Licha ya kujikita kwenye biashara, Joshua anakiri pia anajishughulisha na kilimo.

Anasema analima mahindi na mchele, japo awali alianza kama matumizi ya nyumbani ila kwa sasa anawaza kufanya mazao ya biashara, akijipanga kupata wasimamizi wazuri wa kazi zake.

“Huwa napenda kujaribu kufanya vitu tofauti ilimradi vinakuwa na manufaa. Kilimo nakifanyia mkoani Morogoro. Mwanzo nilianza kama matumizi ya chakula nyumbani, tayari nimezisoma changamoto ambazo zipo kwenye kazi hii, nimeona naweza kuzimudu,” anasema.

ALINUSURIKA KIFO

Katika mahojiano haya, ghafla Joshua anakumbushia tukio la maajabu ambalo kama sio miujiza ya Mungu, sijui leo angekuwa na hali gani ama angekuwa wapi, kwani lilimshangaza na mpaka leo hajajua kama ni la kawaida ama ni michezo ya ‘Kiswahili’.

Anaanza kwa kusimulia tukio hilo, akidai alikaribia kumeza pini iliyokuwa ndani ya wali na hapo sauti yake ilibadilika kama mtu ambaye moyo wake ana uchungu.

Anaongea kwa kituo akiwa amegubikwa na utulivu; “Nakumbuka ilikuwa msimu wa 2011/12 nilihisi ndio mwisho wa maisha yangu, nilienda kwa mama lishe kupiga msosi, si unajua tena haya maisha ya soka letu.

“Kipindi hicho nilikuwa naishi kwenye hosteli za klabu pale Jangwani, ambapo mwanzo tulikuwa tunaweka kambi pale.

“Nikapakuliwa wali na mboga, nikala kijiko cha kwanza, pili, tatu ghafla moyo ukakosa amani, nilipochukua cha nne, kwani ile natafuna ikawa kama kitu kimenichoma, kutema ni pini, aina ile ya zinazotumiwa na kina mama kufungia nepi za watoto.”

Anaendelea kusimulia kuwa, licha ya maumivu aliyoyasikia kwa kujichoma na pini ile kwenye mdomo, lakini alijikuta akitafakari na kujiuliza pini kubwa imekuwaje ikakae kwenye wali? Kisha akaamua kuacha kula msosi ule na kuishia kumshukuru Mungu kwa muujiza huo, kwani anadhani kama ingepitiliza kooni, huenda mambo yangekuwa mengine na hata kufa.

“Pini hiyo nimeitunza kwa sababu ni kitu ambacho sijawahi kupata jibu mpaka leo, ila nashukuru Mungu kwa sababu aliamua kuniepusha na tukio hilo,” anasema.

Anasema pini hiyo ilikuwa imefunguka kiasi kwamba angemeza ingekwama kwenye koo na hivyo maisha yake yangekuwa hatarini.

AJALI NUSURA IUE FAMILIA

Kama hujui Julai 30, 2017 Joshua alibariki ndoa yake jijini Mwanza na anasema wakati anasafirisha familia yake kwenda kufanikisha tukio hilo alikumbana na ajali akiwa amefika katika mkoa huo.

“Nikiwa nimefika Mwanza mjini, moyoni mwangu nikasikia sauti ikiniamrisha nikimbize gari kwa kasi halafu nisipite njia ya kwenda nyumbani, nami nikafanya hivyo bila kusita, huwezi kuamini sekunde chache baada ya kupita eneo hilo kulitokea ajali mbaya na watu waliokuwa kwenye magari yaliyogongana wakafariki hapo hapo. Yaani kama ningekuwa sijakimbiza gari nadhani familia yangu ingefia eneo lile,” anasema.

Anasema baada ya kupona ajali hiyo, siku iliyofuata alifanikiwa kubariki ndoa yake na mwanamke aliyezaa naye watoto wawili ambao ni Mariam ‘Mamu’ (11) na Gaudioza ‘Gaude’ (4).

“Ajali hiyo ni kati ya matukio ambayo sitakaa niyasahau, huwa nasema Mungu akiamua niondoke duniani nitaondoka ila sio kwa kulazimishwa na binadamu,” anasema Joshua ambaye ni mmoja ya wachezaji waliojikita kwenye masuala ya kumcha Mungu.

USAJILI WA SH 25 MILIONI

Joshua anafichua usajili wake ndani ya Yanga mwaka 2010 ulimpa fedha kubwa ya kwanza maishani mwake, kwani alisajili kwa kiasi cha Sh 25 Milioni akitokea Ruvu Shooting na kudumu nayo kwa misimu saba mfululizo kabla ya kuachwa.

Anasema, fedha hizo kwake zilikuwa nyingi na aliamua kuzipeleka kwenye uwekezaji binafsi na nyingine kumgawia baba yake mzazi.

“Tangu naanza kucheza soka, nilikuwa nimeshajiwekea malengo kwa kukumbuka kuwa, kuna kesho ndio maana, nilipopata fedha hizo nilizitumia kwa akili, lakini pia katika maisha yangu yote ya soka sijawahi kuwa na skendo zozote mbaya kwa vile niliiheshimu kazi yangu.”

SOKA LINAMDAI

Mbali na kuishi kwenye mjengo wake na kumiliki magari, anasema soka limemfanyia mambo mengi hivyo anaona linamdai, akiamini siku moja atarejea kivingine.

“Sikutaka kukurupuka baada ya kuachana na Yanga kwenda timu nyingine, niliangalia brandi yangu, sikutaka kwenda kusumbuana na viongozi kudai pesa za mishahara, ndio maana nikaamua kutengeneza pesa,” anasema.

Pia anasema anapenda kuona vijana wanafanikiwa kupitia katika mikono yake, hivyo ameapa kupambana kutimiza hilo.

“Naamini kuna siku nitarejea tena uwanjani kukinukisha, bado nina uwezo hata kama umri umeanza kunitupa mkono,” anasema

YANGA YA MANJI

Anapoulizwa kama kuna tofauti yoyote ya Yanga aliyoichezea na iliyopo sasa, naye anasema ile aliyokuwapo enzi za Yusuf Manji akiwa mwenyekiti, ilikuwa tishio dhidi ya wapinzani katika Ligi Kuu Bara na waliweza kufanya vyema kimataifa.

“Nakumbuka tulichukua ubingwa mara tatu mfululizo, kipindi ambacho Simba ilikuwa inapitia changamoto za hapa na pale, hatukuwahi kulia njaa, wachezaji tulipata kila kitu,” anasema

Anasema Yanga iliyopita ilikuwa tishio kwa sababu ya uwezo wa kiuchumi na hata wachezaji waliosajiliwa walikuwa watu wa kazi kwelikweli na walijitoa ndio maana ilitetemesha hata CAF kwa kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho mara mbili, pia kuvunja utumwa na uteja wa miaka 32 dhidi ya timu za kutoka Afrika Kaskazini, hasa Misri waliowalaza jijini Dar.

AIKUMBUKA AL AHLY

Anasema anaikumbuka mechi dhidi ya Al Alhy ya Misri ambapo kama wangeshinda penalti zao wangetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014.

Mechi hii ndio ambayo ilivunja minyororo ya unyonge wa Yanga dhidi ya Wamisri ambapo bao pekee la kichwa la Nadir Haroub ‘Cannavaro’ liliwazima Al Ahly, lakini nao wakaenda kushinda kwa bao 1-0 na mchezo kwenda hatua ya penalti na Yanga kutoka.

Joshua anasema alikuwa mmoja wa waliokosa penalti sambamba na Mbuyu Twite na Said Bahanuzi na kwamba ilikuwa mechi ambayo walicheza kwenye kiwango cha juu na hata Wamisri hawakuamini kama ni ile Yanga ambao walizoea kuipiga mabao hadi 5-0.

“Tulicheza kwa kiwango cha juu, lakini tukaja kuondolewa kwa penalti, mimi pia nikikosa penalti na nilijisikia vibaya, ila baadaye nikajipa moyo kwamba ni sehemu ya matokeo, hasa baada ya kujua Bahanuzi alikuwa mtu wa mwisho kupiga penalti zile,” anasema.

Hata hivyo, anasema Bahanuzi naye alikosa na timu yao ikatolewa na hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Bahanuzi kuliko mchezaji mwingine yeyote, licha ya wao kumfariji.

YANGA HII ILIKUWA BALAA

Joshua aliyekuwa anamudu beki wa kushooto na kati na wakati mwingine hata mshambuliaji anasema katika kucheza kwake katika mbalimbali ikiwamo Toto, Ruvu Shooting na Yanga kikosi chache bora anakitaja kinaundwa na wachezaji hawa; Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Salum Telela, Idd Athuman ‘Chuji’, Saimon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu na Mbrazil Andrey Coutinho.

“Nimetaja skwadi lote, suala la kupanga nani aanze ama nani akae benchi inategemea aina ya mchezaji na wote tulikuwa na uwezo wa kukupa matokeo mazuri, Yanga hii ilikuwa balaa,” anasema Joshua ambaye alizaliwa miaka 34 iliyopita na kuanza kucheza soka tangu akiwa kinda.

Baadhi ya timu alizozitumikia ni beki huyo wa kupanda mbele ni Toto Africans msimu wa 2006-2008, Moro United 2008-2009, Ruvu Shooting 2009-2010 na Yanga 2010-2017.