Okwi abebeshwa zigo Simba

Muktasari:

  • KOCHA Patrick Aussems wa Simba aliamua kuwapigisha tizi la maana ili kuimaliza AS Vita, huku straika Emmanuel Okwi akibebeshwa mzigo wote wa kumaliza gemu ya kesho Jumamosi Taifa.

KOCHA Patrick Aussems wa Simba kumbe hatanii. Unaambiwa licha ya vijana wake kuchoka kwa safari ndefu kutoka Algeria, kocha huyo aliamua kuwapigisha tizi la maana ili kuimaliza AS Vita, huku straika Emmanuel Okwi akibebeshwa mzigo wote wa kumaliza gemu ya kesho Jumamosi Taifa.

Simba itakuwa wenyeji wa AS Vita katika mechi ya mwisho ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakiwania tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo na Kocha Ausseme hakutaka kulaza damu.

Mbelgiji huyo hakutaka kupoteza muda mara baada ya kutua juzi na jana jioni amewapigisha tizi vijana wake kuwaweka tayari kabla ya kuvaana na AS Vita waliotua usiku wa kuamkia jana Alhamisi na jioni yake nao wakapiga tizi viwanja vya Gymkhana.

Mara baada ya kumaliza mazoezi ya kukimbia na nguvu wakitumia dakika 30, Aussems alihamia katika mazoezi ya mbinu hasa kuchezea mpira akigawa wachezaji wake katika timu mbili tofauti.

Timu ya kwanza ilikuwa na kipa Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Mohammed Ibrahim, Haruna Niyonzima, Adam Salamba na Rashid Juma.

Nyingine walikuwepo kipa Ally Salim, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Yusuph Mlipili, Poul Bukaba, James Kotei, Mzamiru Yassin, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.

Katika zoezi hili Aussems alitaka kila mchezaji aguse mpira usizidi mara tatu, lakini ili wapige pasi nyingi tena kwa haraka na wakitengeneza nafasi kupitia kwa viungo wa kati na pembeni kupitia kwa mawinga na mabeki wa kushoto na kulia.

Katika kila timu iliyokuwa inafanya vizuri Aussems na msaidizi wake, Dennis Kitambi walionekana kufurahishwa kwa kuwapongeza na wale waliokuwa wanakosea alikuwa akisimamisha mpira kisha anamuelekeza cha kufanya wakati huo.

OKWI ABEBESHWA MZIGO

Katika zoezi hilo la kucheza timu mbili tofauti ambalo walitumia nusu uwanja baada ya kuweka goli dogo katikati lilimalizika timu kwa kwanza kushinda bao 1-0, ambalo lilifungwa na kiungo Haruna Niyonzimakwa mkwaju wa penalti baada ya Mlipili kunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Zoezi hilo lilionyesha Okwi ambaye alikosekana katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo walipoteza kwa kufungwa mabao 2-0, nchini Algeria amerudi tena akiwa fiti na mzuka wa kuwamaliza AS Vita.

Okwi alionyesha yupo fiti baada ya ule ubora wake wa kupiga chenga nje ya boksi na kumlazimisha beki kumwingiza ndani ya eneo la hatari na kupiga mashuti ya maana kwani aliweza kufanya hivyo kwa Coulibaly na mashabiki waliokuwa uwanjani hapo kumpigia shangwe na kumshangilia.

Mbali ya kuonyesha hilo Okwi alicheza kwa maelewano na washambuliaji wenzake Kagere na Bocco ambao walionekana wakitengenezeana nafasi huku sura zao zikiwa na furaha muda wote walipofanya zoezi hilo.

Aussems alisema kurudi kwa Okwi ambaye ameonekana kuwa fiti ni habari njema kwa benchi la ufundi na mashabiki kuelekea katika mchezo mgumu ambao utahamua hatma yao ya kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Kama Okwi ataendelea kuwa fiti na kuimalika kama alivyofanya katika mazoezi ya leo ni habari njema kwetu kuelekea katika mchezo huo mgumu kwani ni kitu kizuri kuwa na mchezaji mzoefu aina yake ambaye anaweza kuamua mechi,” alisema Aussems.

Naye beki kiraka Nyoni alionekana kurejea mazoezini akiwa fiti akifanya mazoezi ya nguvu pamoja na wenzake na muda wa kucheza timu mbili alichezeshwa katika eneo la ulinzi ambalo alikuwa akishirikiana na vyma na Wawa.

Kocha Aussems alisema wanakwenda kucheza mechi ambayo itakuwa historia kwa klabu yake lakini anachofahamu wanapocheza katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam, si kitu rahisi kwa timu yoyote kuweza kuifunga Simba.

Alisema benchi la ufundi na wachezaji wote tunatambua umuhimu wa mechi hii ambayo kwangu nitakwenda kucheza kwa kufunguka na kushambulia ili kutimiza lengo la kushinda na kusonga mbele ndio maana hapa katika mazoezi tumefanya mazoezi ya nguvu ili wachezaji kuwa fiti muda wote na yale ya mbinu katika kushambulia.

“Naweza nikamtumia Okwi na Juuko wakamaliza dakika zote 90 au wasimalize kutokana wametoka katika maumivu lakini uwepo wao wote wakiwa fiti kwetu ni jambo zuri ambalo tuna imani watatoa mchango mkubwa ndani ya timu na kupata matokeo ya uushindi ambayo tunaamini tutapata.”

“Simba ina rekodi nzuri katika mechi zote za nyumbani si msimu huu hata mechi za nyuma katika mashindano haya makubwa nina imani na naona nafasi ya kufuzu kwa kiasi kikubwa kwani tuna kila sababu ya kulitimiza hilo ingawa tunacheza na timu nzuri na kubwa hapa Afrika,” alisema Aussems.