Njooni Kwa Mkapa tumalize mambo!

Njooni Kwa Mkapa tumalize mambo!

“MSIMU uliopita tuliondolewa katika mashindano haya kwenye hatua ya awali na UD Songo ya Msumbiji kwa faida ya bao la ugenini, lakini kutokana na sababu mbalimbali zilizotukwamisha.

Kukwama kupata matokeo mazuri ambayo yangetuvusha katika hatua ya mbele kama wapenzi wengi wa soka hapa nchini walikuwa wakifikiria hivyo, ilimuumiza kila mmoja.

Jambo la kwanza ambalo lilitukwamisha kupata matokeo mazuri ni kwamba tulikuwa tumetoka katika maandalizi ya msimu mpya amabao tulifanya mazoezi mengi magumu na ilitakiwa tupate muda wa kutosha wa kupumzika ili miili yetu kurudi katika hali ya ushindani.

Tukiwa tunajipanga katika ratiba hiyo tutakutana na michuano ya Caf dhidi ya timu ambayo ligi yao ilikuwa inaelekea ukingoni kwa maana walikuwa katika hali ya ushindani, huku tukiwa bado hatujachanganya hiyo ni moja ya sehemu ambayo walituzidi.

Jambo lingine, kikosi chetu kilikuwa na maingizo ya wachezaji wapya waliokuwa hawajazoea mazingira ya timu na walikuwa wakipewa nafasi ya kucheza katika timu na kabla hatujazoeana tukakutana na mechi ngumu ambayo inahitaji mbinu na akili.

Msimu huu mbali ya changamoto hizo ambazo nimezieleza na ambazo sijazieleza lakini tulikutana nazo msimu uliopita mpaka tukaondolewa katika hatua ya awali tumejipanga mapema kuzifanyia kazi ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.

Miongoni mwa eneo ambalo tumeimalika kikosi chetu kinawachezaji wazuri ambao wamekaa kwa pamoja tangu msimu uliopita na wale wachache ambao wamesajiliwa msimu huu wamekuja kuongeza nguvu pale palipokuwa na mapungufu ambayo tulionyesha msimu uliopita.

Ukiangalia ligi yetu tayari imeshachanganya na tupo katika mzunguko wa 13, ambao wachezaji wengi wamepata kutumika na kucheza kwa kuzoeana kwa maana hiyo hata kocha amepata uwanja mpana wa kuamua kundi gani la kuwatumia kutokana na wapinzani wetu walivyo.

Miongoni mwa silaha yetu nyingine ni kucheza vizuri katika uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa na hapo huwa tunakuwa na morali ya aina yake kutokana na wengi wa mashabiki wetu jambo ambalo wachezaji tunapata morali ya kutosha dhidi ya wapinzani ambao lazima wataingiwa na hofu ya kuacha pointi tatu.

Silaha hii ya uwanja wa nyumbani misimu miwili iliyopita tulishindwa kuitumia baada ya kuondolewa na TP Mazembe katika hatua ya robo fainali baada ya kutoka nao suluhu nyumbani kabla ya kutufunga katika mechi ya maruadiano na msimu uliopita UD Songo ilipata sare ya bao 1-1 kwetu wakatuondoa kwa sheria ya bao la ugenini.

Msimu huu tumedhamiria vizuri kutumia uwanja wa nyumbani na baada ya hapo tutakuwa tukicheza kwa nguvu na nidhamu kubwa tutakapokuwa ugenini kama ambavyo tulifanya katika mechi ya mzunguko wa kwanza na Plateau United kule kwao Jos Nigeria.

Katika dhana hiyo tunatambua tunakwenda katika mchezo mgumu wa marudiano lakini akili kubwa ni kuhakikisha tunakuwa na nidhamu na wapinzani kwani si wabaya kutokana na ambavyo wamecheza nyumbani kwao lakini naimani kuwa tutapata pointi ushindi dhidi yao.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf), wametupa ruhusa ya kuingiza mashabiki nusu ya uwanja hii ni faida ambayo timu nyingi za Afrika haipati kutokana na kujikinga na janga la virusi vya corona kwa maana hiyo kadri tulivyoruhusiwa kuingiza mashabiki waje watushangilie mwanzo mwisho.

Kwa mfano nikiwa nacheza uwanjani kuna mashabiki wengi ambao wanashangilia timu yangu nakuwa na hamasa kubwa ya kutaka kupambana na kujitolea mwanzo mpaka mwisho wa mechi ili kupata kile ambacho kinahitajika lakini naamini si kwangu tu, hilo bali kwa wachezaji wengine wote.

Ukiangalia wachezaji wetu mmoja mmoja morali inaonekana kuwa juu katika mechi hiyo ya marudiano ili kuhakikisha tunachukua ushindi hapa nyumbani na kusonga katika hatua inayofuata ili kuwa njia na kufikia malengo yetu ya kufika mbali.

Unajua mashindano haya ni mabingwa tu ambao wanatoka kila nchi kwa maana hiyo hakuna timu ambayo inacheza huku ikiwa haipo vizuri kutokana na matokeo ambayo wameyapata katika mechi ya ugenini tunalitambua hilo na tunakwenda kulifanyia kazi huku tukiamini itakuwa siku ya furaha kwetu kwa kuondoka na ushindi.

Bao moja ambalo tumefunga ugenini wala hatutaliwazia kutokana mechi hiyo imeshamalizika na sasa nguvu na akili ni kuanza upya mchezo wa Jumamosi ambao tunatambua wapinzani watakuja na lengo la kutaka kusawazisha makosa jambo ambalo naimani linawezekana.

Kushinda kwa mechi hiyo maana yake tutasonga katika hatua inayofuata ambayo ndani yake kuna mianya mingi itafunguka kama timu kwenda mbele ambapo kuna zawadi kama motisha zinatoka kutoka Caf, lakini ndani ya timu kwa viongozi wetu kama bonasi.

Nchi nayo inaweza kufanikiwa kwa kupata pointi ambazo zinaweza kutoa fursa ya kuongeza timu katika mashindano hayo kama ilivyokuwa mwaka juzi lakini kwa wachezaji inaweza kuwa faida kwao wakapata nafasi ya kuonekana katika maeneo mengine.

Kuna baadhi ya wachezaji wengi wamenufaika kupitia mashandano haya kwa maana ya kusajiliwa na timu nyingine kwa pesa nyingi, kuitwa au kupata nafasi ya kucheza katika timu yako ya taifa, kupata tuzo mbalimbali ambazo zinaweka heshima kwa mchezaji na mambo mengine mengi.

Kwa maana hiyo mechi ya marudiano ya Plateau United tutaitolea macho kama tunacheza fainali ili kupata ushinda na kusonga mbele kama malengo yetu ya mashindano haya yalivyo msimu huu.