Ni shoo ya Kagere, Dilunga

MASTAA wa Simba, Hassan Dilunga na Meddie Kagere wanaonekana kuwa na kitu muhimu cha kuibeba timu katika mechi ya watani wa jadi itakayopigwa Desemba 11 ingawa Yanga wanaonekana kuwa bora zaidi.

Dilunga na Kagere wamekuwa wakitajwa zaidi kwa sasa kutokana na viwango vyao walivyovionyesha kwenye mechi za hivi karibuni ikiwemo ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ambao wametolewa.

Kuelekea mechi yao ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, nyota hao wanaonekana kuwa mwiba kwa wapinzani wao ingawa pia imeelezwa lolote linaweza kutokea.

Wakizungumza na gazeti hili, Kocha wa Mwadui FC, Mohamed Rishard ‘Adolf’ alimwelezea Dilunga ameisaidia Simba kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kufunga bao ugenini dhidi ya Red Arrows, matokeo yakimalizika kwa kufungwa mabao 2-1.

Alisema Dilunga anajua kukaa na mpira mguuni na kuukokota, jambo analoona huduma na kiwango chake kitakuwa chachu ya kuibeba timu yake.

“Dilunga analeta chachu kwenye timu, kikubwa atunze nidhamu ya kazi itakayofanya aendelee kucheza kwa kiwango cha huduma yake kuwa muhimu kikosi cha kwanza, kiufundi amekomaa,” alisema Adolf na akaongeza;

“Nimewahi kumfundisha timu ya taifa ya vijana, nyakati hizo walikuwa wanatoka timu moja na Mbwana Samatta na Frank Domayo, walikuwa vijana wenye vipaji vya juu, kilichokuwa kinamkwamisha ni nidhamu ya kazi yake tu ndio maana nasisitiza aitunze,” alisema.

Ukiachana na Dilunga alimzungumzia Kagere kwamba, bado anaamini ni straika mzuri, isipokuwa kuna nyakati za mpito ambazo hazimaanishi kaishiwa kiwango.

“Sitaki kumzungumzia ameshuka, ikumbukwe huyo ndiye alikuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo, ligi inayoendelea ana mabao manne, hivyo anaweza akafanya lolote la kurejesha jina lake juu,” alisema.

Kwa upande wa staa wa zamani wa Yanga, Idd Moshi alisema; “Ni kweli Dilunga ama Kagere wanaweza wakawa vizuri ama kwa Yanga Fiston Mayele na Jesus Moloko wakawa vizuri ila dabi haina fundi, itategemeana na mchezaji atakayeamka vyema ndiye atapata heshima mbele ya mashabiki wake.”

Aliyekuwa kocha msaidizi wa Jackson Mayanga katika timu za Kagera Sugar na KMC, Mlage Kabange alisema Dilunga kwa sasa yupo kwenye kiwango kikubwa, anachotakiwa aamue kujitoa mhanga ili awe na muendelezo wa kile kilichowafurahisha mashabiki.

“Jambo la msingi analotakiwa kulifanya Dilunga, azingatia miiko na nidhamu ya kazi, ili mguu wake uendelee kutema madini, upande wa Kagere ni mpambanaji asiyekubali kushindwa, anaweza akafanya kitu kwenye mechi hiyo na ndiye straika anayetegemewa,” alisema.

Kuhusu kiwango cha Simba kuelekea mchezo huo, mchezaji wa zamani na mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema; “Simba kuingia hatua ya makundi kumewarejesha mchezoni, hivyo mchezo utakuwa 50/50.”

Kocha wa zamani wa Stand United na Gwambina FC alisema itakuwa dabi ya kwanza yenye ufundi mwingi zaidi na mechi ya aina yake kwani vikosi vyote vina nguvu.