‘Ni Fei Toto na Mzize tu’

Muktasari:
- Mbali na Fei Toto, Juma pia amesema Clement Mzize wa Yanga naye amefanya kazi kubwa ikingatiwa ndiye kinara wa mabao kwa wazawa.
MSHAMBULIAJI wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma amesema kati ya wachezaji wazawa waliofanya vizuri kwa msimu huu ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayeitumikia Azam.
Mbali na Fei Toto, Juma pia amesema Clement Mzize wa Yanga naye amefanya kazi kubwa ikingatiwa ndiye kinara wa mabao kwa wazawa.
Msimu huu Fei Toto anaongoza kwa asisti akiwa nazo 13, huku akifunga mabao manne. Ikumbukwe kuwa msimu uliopita nyota huyo alimaliza ligi na mabao 19 nyuma ya kinara Aziz Ki aliyekuwa Yanga na mabao 21.
Kwa upande wa Mzize ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao sita na asisti saba katika Ligi Kuu Bara akicheza kwa dakika 1299, msimu huu umekuwa bora zaidi kwani hadi sasa ana mabao 13 na asisti nne akicheza mechi zote 27 kwa dakika 1,678.
Akiwazungumzia wachezaji hao, Juma alisema: “Kwanza ni wachezaji vijana wanaojituma kwa nidhamu ya juu, kikubwa waendelee kulinda viwango vyao vitakavyowafanya kuwa ghali katika soko la usajili, ndiyo maana wote wawili wanatakiwa na klabu mbalimbali za ndani na nje.”
Alisema wachezaji hao nje na kuzisaidia timu zao, wana faida kubwa kwa timu ya Taifa, huku akiwashauri nguvu zao wazielekeze katika kazi na siyo mashabiki wanaoweza kuwatoa mchezoni wakati wowote.
“Kuna muda wachezaji wa kigeni wanacheza kwa uchoyo, akifanya Mzize unaona mashabiki wanavyomshambulia na kusahau, anapaswa kujengwa siyo kwa ajili ya timu yake pekee bali kuisaidia Taifa Stars,” alisema Juma ambaye alikiri msimu huu kwake ni mbaya kutokana na kuuguza majeraha kwa muda mrefu.
Katika mechi chache alizocheza mshambuliaji huyo msimu huu amefunga bao moja dhidi ya JKT Tanzania, huku matarajio yake ni kuona Tanzania Prisons ikisalia Ligi Kuu.
“Nimeishapona, naamini tukisalia Ligi Kuu msimu ujao nitafanya kitu kikubwa ikiwemo kuifikia rekodi yangu ya mabao 15 niliyofunga msimu wa 2017/18,” alisema.