Ndayiragije: DRC imenipatia kikosi

Wednesday January 13 2021
ndayiragije pic
By Thomas Ng'itu

Dar es Salaam. Kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Ettiene Ndayiragije amesema amepata kikosi kwa ajili ya Fainali za Wachezaji wa Ndani barani Afrika (Chan), baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, jana.

Katika mchezo huo timu hizo ziliofungana bao 1-1, Stars ililazimika kusawazisha bao baada ya kipindi cha kwanza kumalizika ikiwa nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa na Mayele Kayala katika dakika ya 19.

Mchezo huo ambao pia ulikuwa mahususi kwa ajili ya kumuaga beki wa kati wa timu hiyo, Aggrey Morris, Stars ililazimika kurejea kipindi cha pili kwa kasi na hasa baada ya kuingia kwa Ditram Nchimbi ambaye katika dakika ya 51 alitoa krosi kutokea kulia iliyofikia kichwani kwa Ayoub Lyanga aliyeukwamisha mpira wavuni.

Akizungumza baada ya mchezo, Ndayiragije alisema: “Kikosi nimepata..ndiyo nimepata kikosi.”

ndayiragije pic 1

Hata hivyo, kocha huyo hakufafanua ni wachezaji gani atakaoambatana nao Cameron kushiriki Chan, badala yake alizungumzia mchezo huo akisema walilazimika kurejea kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha bao.

Advertisement

“Tunashambulia kama timu na tunalinda kama timu,” alisema kocha huyo.

Naye Morris akizungumzia uamuzi wa kustaafu Stars alisema: “Vijana wanachipukia na huu ndio muda (wangu) sahihi wa kupumzika,” alisema. Kabla ya mchezo huo mchezaji huyo alikabidhiwa zawadi ya jezi ya Taifa Stars iliyosainiwa na wachezaji wote pamoja na mfano wa hundi ya Sh5 milioni aliyokabidhiwa na rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Advertisement