Nabi fasta abadili kikosi Yanga, Senzo aipeleka makundi

Nabi fasta abadili kikosi

YANGA imekiri hatua inayofuata wanakwenda kushindana na timu bora na ngumu zaidi na fasta kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amethibitisha kukifumua kikosi hicho kwa mechi hizo ili kuhakikisha wanatoboa hadi makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu.

Wababe hao wa Ligi Kuu Bara, waliitupa Zalan ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0, ikishinda mechi ya kwanza ya ugenini 4-0 na juzi ikiwa nyumbani ikaongeza dozi na kuwa 5-0 na sasa itavaana na Al Hilal ya Sudan.

Mara baada ya kujihakikisha kwenda raundi ya kwanza, Kocha Nabi aliliambia Mwanaspoti, kikosi kitakachokutana na Al Hilal kitakuwa tofauti kabisa na hiki kilichoinyoosha Zalan.

Nabi alisema ameshazisoma timu zote hizo na kazi hiyo ilikuwa ikiendelea jana usiku zilipokuwa zikirudiana Mjini Khartoum Sudan, ambapo wenyeji waliopasuka mchezo wa kwanza wakiwa ugenini.

Kocha huyo aliyeiongoza Yanga katoka mechi 41 za Ligi Kuu Bara tangu Aprili mwaka jana bila kupoteza, alisema kwenye mechi hizo watakuwa na mfumo tofauti na hata upangwaji wa kikosi chao.

“Najua mashabiki hawajafurahia tunavyopoteza nafasi, hata mimi naungana nao lakini hili limetokana na wachezaji kupania kumaliza mechi mapema wakajikuta wanajiweka katika presha tutalifanyia kazi hili, sio kila mechi utapata nafasi nyingi kama hivi,” alisema Nabi na kuongeza;

“Hatua inayofuata itakuwa ngumu kwani tutaenda kukutana na watu bora kama ilivyo sisi, najua tutakachofanya tutakuwa na muundo tofauti kabisa kuanzia nidhamu yetu hata upangwaji wa kikosi.”

Nabi aliongeza; “Kuna aina ya mpinzani anakulazimisha kujiachia, ila kuna timu inakulazimu kujihadhari ili usijiweke katika mazingira magumu kitu tunachoomba sasa ni kuimarika kwa wachezaji ambao walipata majeraha katika mechi hizi tatu.”


MSIKIE SENZO

Wakati Nabi akiyasema hayo aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Yanga, Senzo Mazingisa ameliambia Mwanaspoti kwa simu kutoka Sauzi, kuwa anafuatilia mechi zote za timu hiyo na anaamini inatinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Senzo ambaye aliachia ngazi wiki chache kabla ya msimu mpya kuanza alisema Yanga iko moto na ubora wa kikosi chao na benchi lao la ufundi siyo sawa na St George wala Al Hilal wataweza kuwazuia wasiende makundi kama wachezaji watajituma uwanjani kwenye mechi zijazo.

“Naamini kutakuwa na mipango mikubwa kuelekea hizi mechi mbili zinazofuata, nafuatilia mechi za Yanga unajua mimi ni mwananchi timu iko moto sana,” alisema Senzo ambaye aliiongoza Yanga kuchukua mataji matatu msimu uliopita.

“Kikosi kimejaa vizuri sidhani kama ni suala la Zalan dhaifu pekee, hiki ni kikosi ambacho kimeshinda mechi nyingi ngumu, pia kuna benchi bora la ufundi hivi ni vitu vinavyoitofautisha Yanga na timu itakayokutana nayo hatua inayofuata, nawaona Wananchi wakitinga hatua ya makundi msimu huu.”