Nabi afunguka, Prisons wacheka

Thursday May 12 2022
Nabi PIC
By Thomas Ng'itu

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ameweka wazi anachokwenda kukifanya mazoezini kuanzia leo jioni lakini Prisons nao wakagusia walivyoidhibiti mechi ya juzi.

Yanga imecheza mechi tatu mfululizo bila kupata bao huku wakiwa na mshambuliaji Fiston Mayele ambaye ana mabao 12 na kwenye msimamo wa wafungaji.

Akizungumza baada ya mchezo wao na Prisons kumalizika, Nabi alisema; “Tulitengeneza nafasi nyingi sana na wachezaji walikosa, Makambo (Heritier), Feisal (Salum) na Moloko (Jesus) wote hawakufunga licha ya kuwa kwenye nafasi nzuri.”

“Bado tuna nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa msimu huu, nina uzoefu mkubwa na unapotaka ubingwa lazima ujifikirie wewe mwenyewe na sio timu unayoshindana nayo.”

Aliongeza kwamba anakwenda kufanya kazi kubwa kwenye uwanja wa mazoezi.

Katika suluhu dhidi ya Prisons, Yanga ilipata penalti na kupiga Mayele ambaye hajawahi kupiga penalti ndani ya dakika 90 na alipopiga mpira huo alipaisha na kuzidi kumuongezea presha.

Advertisement

Akizungumzia tukio hilo Nabi alisema: “Mayele sio kama alichukua yeye ule mpira bali wenzake ndio walimtaka apige na ikatokea vile, haitakiwi atupiwe lawama yeye na kumtoa mchezoni.”

Nabi aliongeza: “Mabadiliko ya Sure Boy sio kwamba alicheza vibaya, alicheza vizuri lakini alikuwa amechoka kidogo na nilimtoa ili kutafuta bao kwenye mchezo, kama nilivyomtoa Kibwana (Shomari) na kuingia Farid (Mussa) lakini bado haikuzaa matunda.”


PRISONS WALICHOFANYA

Kocha mkuu wa Prisons, Patrick Odhiambo amesema siri kubwa ya kupata suluhu katika mchezo wao dhidi ya Yanga ni kujua namna ya kubana mashambulizi ya wapinzani wao.

“Yanga inatumia zaidi upande wa Djuma (Shaban) na mimi kule niliwaweka wachezaji wawili ambao niliona kabisa wana nguvu za kumzuia,” alisema Odhiambo.

“Alicheza Benjamin Asukile kama winga (nafasi yake ni beki) pamoja na Ibrahim Abraham na walikuwa kwenye maelewano makubwa ya kuubana upande ambao tulijua una madhara.”

Akizungumzia upande wa kumbana mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, kocha huyo alisema alitoa maelekezo kwa mabeki wake na walifanikiwa.

“Nilimuambia Chona (Nurdin) awe makini na Mayele kwa sababu akiwa ndani ya boksi ni mzuri sana kwenye kufunga, aliweza kumbana kwa dakika zote,” alisema.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa soka msimu huu umekuwa na ushindani mkubwa kutokana na hali ya kiuchumi ya timu mbalimbali ambazo zinaweza kujikimu.

Advertisement