Nabi afanya umafia, amteka straika mpya Simba

Nabi afanya umafia, amteka straika mpya Simba

SIMBA inapambana kumaliza usajili wa kinara mmoja wa mabao ambaye klabu yake inaweka ngumu, lakini kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amefanya umafia akijifungia na staa huyo kupiga stori.

Nabi juzi alifanya umafia huo mbele ya mabosi wa Simba akijifungia kwa nusu saa na mshambuliaji Cesar Mazoki anayeichezea Vipers ya Uganda.

Iko hivi. Nabi alifika hoteli moja ambayo walifikia Vipers ambao ni walikuwa wageni wao kisha akamchomoa Mazoki mbele ya mabosi wa Simba.

Manzoki haraka aliingia ndani ya gari la Nabi, kisha wawili hao ambao wanajuana kitambo waliteta kwa takriban dakika 30 ndani ya gari moja ndogo ya kisasa ambayo kocha bora huyo nchini alipewa na tajiri wa Yanga, Ghalib Said ‘GSM’.

Kabla Nabi hajafika hotelini hapo Mazoki alikuwa katika kikao na mabosi wa Simba akiwemo Crenstencius Magori ambaye baadaye alishtuka kumuona mshambuliaji huyo anachelewa kurudi.

Wakati Magori akimsaka ghafla akamuona Mazoki akishuka kwenye gari ambapo kigogo huyo alipoichunguza kwa haraka akamuona Nabi akiondoka kwa haraka eneo hilo.

Hata hivyo, haikujulikana mara moja Nabi alikuwa akiteta nini na mshambuliaji huyo, lakini Mwanaspoti linafahamu wawili hao ni marafiki wa muda mrefu.

Hatua hiyo iliwashtua Simba na Magori alilazimika kuchelewa kuondoka katika hoteli hiyo ili kuhakikisha mshambuliaji anabaki salama katika mikono yao, huku ikielezwa kuwa atajiunga na Simba kwenye dirisha dogo lijalo baada ya dili la sasa kukwamishwa na mabosi wa Vipers yenye mkataba naye.