'Msije uwanjani mtaumbuka'

Mashabiki wa Klabu ya Simba. PICHA|MAKTABA
Muktasari:
- Habari zinadai kwamba hata mashabiki wa tawi la Yanga ndani ya kituo cha Ubungo nao wamejitolea kuwaongezea nguvu Stand kuhakikisha Simba inatoka sare au kupoteza mchezo huo ili wachanganyikiwe kisaikolojia kabla ya kucheza na Yanga Oktoba 18.
STAND United ipo Tandika jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya wiki sasa wakijiandaa na mechi dhidi ya Simba itakayochezwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa. Timu hiyo ya Shinyanga imekuwa ikifanya mambo yake kwa siri kwa kuhofia wachezaji wake kurubuniwa na mashabiki wa Simba ambayo imepania kwa udi na uvumba kupata ushindi wa kwanza baada ya sare mbili mfululizo.
Taarifa rasmi zinasema mashabiki zaidi ya 200 kutoka vituo mbalimbali vikubwa vya mabasi wametua Dar es Salaam kuunganisha nguvu na wale wa kituo cha Ubungo Terminal kuhakikisha timu yao inashinda. Habari zinadai kwamba hata mashabiki wa tawi la Yanga ndani ya kituo cha Ubungo nao wamejitolea kuwaongezea nguvu Stand kuhakikisha Simba inatoka sare au kupoteza mchezo huo ili wachanganyikiwe kisaikolojia kabla ya kucheza na Yanga Oktoba 18.
Lakini Simba ambao pia wana tawi kituoni hapo wameshtukia mchezo wote wa mashabiki wa Yanga na Stand na kuwatamkia kwamba; “Msije Uwanjani mtaumbuka.”
Simba imesisitiza kwamba kwa vyovyote vile lazima waikung’ute Stand ili waingie na morali na nguvu mpya kwenye mechi ya watani wa jadi ambayo itagonganisha utaalamu wa Makocha Patrick Phiri na Marcio Maximo.
Simba inarejea Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kusaka ushindi wa kwanza ambapo kocha Phiri anasema; “Kila unapozungumza na shabiki hata kiongozi wa timu kila mmoja anataka kuona tunashinda mchezo huu wa Stand, huwezi kukutana na mtani wako ukitokea katika matokeo ambayo hayafurahishi. Tutakutana na Yanga baada ya kumalizana na Stand ni vyema tukipata ushindi.”
“Tumekuwa na siku sita za maandalizi, tumefanya juhudi kubwa kuyafanyia kazi upungufu wetu tuliobaini huko nyuma, siwafahamu Stand ila tunawaheshimu, nimewaambia wachezaji wangu kwa kuwa Stand imepanda ligi ni lazima itatukamia wanatakiwa walitambue hilo,” alisisitiza kocha, ambaye anafikiria kusajili wachezaji wapya watatu kwenye dirisha dogo la Desemba.
Stand United huenda ikakabiliwa na wakati mgumu kwenye dakika 45 za kwanza za mchezo huo kutokana na kwamba wachezaji wake wote wanacheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo mkubwa na wa kisasa, hawajazoea utitiri wa mashabiki na kelele za uwanja huo lakini vilevile hawajazoea mechi kubwa hivyo Simba huenda wakatumia faida hiyo kipindi cha kwanza. Hata ushamba wa jiji huenda ukawaathiri ingawa kipindi cha pili wanaweza kurejea na nguvu za ajabu.
Kocha mkuu wa Stand, Emmanuel Massawe alisema jana ; “Mechi hii itakuwa rahisi tu kwetu muhimu ni pointi tatu hakuna kingine tumejipanga hakuna majeruhi wowote mpaka sasa tunasubiri muda ufike tuingie uwanjani.”
Naye kocha msaidizi wa timu hiyo Athumani Bilali alisema hana wasiwasi na mchezo huo kwa kuwa mara nyingi akicheza na timu hiyo huwa haimsumbui na anawajulia vilivyo.
Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 na Coastal Union na baadaye bao 1-1 na Polisi Moro wakati Stand wao walifungwa mabao 4-1 na Ndanda mkoani Shinyanga kabla ya kuifunga Mgambo JKT bao 1-0 wikiendi iliyopita.
Prisons v Azam
Maafande wa Prisons watakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Azam FC, mkoani Mbeya katika mchezo mwingine wa ligi. Prisons inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Yanga wakati Azam inaingia ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Ruvu Shooting wikiendi iliyopita.
Kocha wa Prisons, David Mwamwaja alisema, “Tumejiandaa vizuri kuhakikisha kuwa tunapata ushindi wetu wa pili wa ligi, natambua kuwa Azam ni timu nzuri lakini nimewatengeneza wachezaji wangu kwa mapambano,”
Kocha msaidizi wa Azam, Ibrahim Shikanda alisema, “Tuliitazama Prisons wakati ikicheza na Yanga wikiendi iliyopita, ni timu nzuri na inaonekana imejipanga vizuri msimu huu.”
Ruvu Shooting v Mbeya City
Mashabiki 200 wa Mbeya City wametua Pwani wakiwa na mabasi matatu kuipa nguvu timu yao itakapocheza dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa Mabatini. Mwenyekiti wa Tawi la Mashabiki Uhindini, Madili Asajile alisema mashabiki wa Dar es Salaam na wataungana na kuwapa nguvu.
“Msimu uliopita tulikuwa na idadi ndogo ya mashabiki wanawake waliokwenda kuishabikia timu ikiwa nje ya mkoa wetu, lakini timu ikicheza kwetu wanakuwa wengi, hivyo mwaka huu nao wajipange vizuri,” alisema Katibu wa Mashabiki wa Tawi la Sido, Raysir Ngelangela.
Ruvu Shooting watakuwa na kazi nzito wakisaka ushindi wa kwanza baada ya kupoteza mechi mbili za awali na wako mkiani mwa msimamo wa ligi.
Polisi v Kagera
Maafande wa Polisi Morogoro watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kuwakaribisha Kagera Sugar leo Jumamosi. Polisi inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba wikiendi iliyopita wakati Kagera wao wanaingia kifua mbele baada ya kuifunga JKT Ruvu mabao 2-0 wikiendi hiyo.
Kocha wa Polisi, Adolf Rishard alisema, “Tunafahamu kuwa Kagera ni timu nzuri na imekuwa na ushindani mkubwa hivyo mchezo huo utakuwa ni mgumu sana lakini tutajitahidi kuhakikisha hesabu zinakuwa upande wetu.”
Coastal v Ndanda
Mkoani Tanga, Coastal Union itakuwa wenyeji wa Ndanda ya Mtwara kwenye mchezo wao wa tatu wa Ligi leo Jumamosi. Coastal inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 na Mbeya City wakati Ndanda inaingia ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Mtibwa Sugar wikiendi iliyopita.
Awali Ndanda ilikuwa ikiongoza ligi baada ya kuifunga Stand United mabao 4-1 kwenye mechi ya kwanza ya Ligi wakati Coastal Union ikitoka sare ya mabao 2-2 na Simba kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mtibwa v Mgambo
Mtibwa Sugar bado itaendelea kucheza kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Manungu, Turiani Morogoro katika mchezo wake wa tatu wa ligi itakapowakaribisha Mgambo JKT kesho Jumapili. Mtibwa inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda na 2-0 dhidi ya Yanga wakati Mgambo itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United na ushindi kama huo kwenye mchezo wake wa kwanza wa ligi ilipoifunga Kagera Sugar.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Maxime alisema, “Kwa sasa kila mchezo tunaupa uzito sawa na mazoezi yetu yamekuwa makali, tulipoteza mchezo kwa Mgambo msimu uliopita lakini kwa sasa hatutaki kabisa hayo yajirudie, tumejipanga kushinda ili tujiweke pazuri kwenye msimamo.”
Kocha wa Mgambo, Bakari Shime alisema, “Mpira ni mchezo wa makosa, tulipoteza mchezo uliopita kwa makosa madogo madogo ambayo tumeyarekebisha na tumejipanga kupambana kuhakikisha tunapata ushindi bila kujalisha tunacheza nyumbani ama ugenini.”
Yanga v JKT Ruvu
Yanga baada ya kufungwa katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar na kujifariji kwa pointi tatu walizovuna katika mchezo dhidi ya Prisons yenyewe chini ya Mbrazil wake Marcio Maximo itashuka kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kesho Jumapili kucheza na JKT Ruvu wenye pointi moja baada ya kutoka suluhu mchezo wao wa kwanza dhidi ya Mbeya City na baadaye kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Kagera Sugar.
Ushindi wa mabao 2-1 walioupata katika mchezo wa Prisons haukumfurahisha Maximo, ambaye baada ya matokeo hayo amekuwa mkali kwa wachezaji wake akiwatupia lawama kwa kucheza chini ya kiwango ambapo tayari ameonekana kufanya uamuzi mgumu kwa kumuondoa mshambuliaji wake Mrisho Ngassa katika mipango ya kikosi cha kesho kwamba hakabi nafasi ambayo sasa atakabidhiwa Simon Msuva.
Habari njema kwa timu hiyo ni kupona kwa beki wake wa kushoto Oscar Joshua aliyekuwa majeruhi sambamba na washambuliaji Hussein Javu na Mbrazil Genilson Santos ‘Jaja’ ambao wote wamefanya mazoezi makali jana tayari kwa mchezo huo.
Wakati Yanga ikijipanga hivyo Ruvu nao kupitia kocha wao mkuu Fred Minziro kwanza ameukana urafiki na klabu yake hiyo za zamani akisema Yanga haimhusu na kesho Jumapili atathibitisha hilo uwanjani kwa kuhakikisha wanapata ushindi na kuondoka na pointi tatu.
“Sina urafiki na Yanga mimi ni kocha wa Ruvu (JKT) na hao wanaosema Yanga nawaachia hayo ni maneno yao, tupo sawa, vijana wangu wako sawa tumejipa kupata ushindi ingawa tunatambua kwamba tunakutana na timu nzuri iliyofanya usajili mkubwa,” alisema Minziro.