Moto vita ufungaji Ligi ya Wanawake

Dar es Salaam. Katika Ligi Kuu Bara ya Wanawake vita ya ufungaji bora imepamba moto kwani wachezaji wa timu mbalimbali wamepania kutwaa kiatu cha dhahabu msimu huu.

Achana na mauaji ambayo Simba Queens iliifanyia ES Unyanyembe kwa kuichapa mabao 16-1, habari kubwa ni jinsi mshambuliaji wa timu hiyo, Oppah Clement alivyofunga magoli sita katika mchezo huo na hivyo kumfukuzia kwa kasi kinara wa mabao kwenye ligi hiyo, Fatuma Mustapha wa JKT Queens.

Oppah alifunga mabao hayo katika mchezo huo na kufikisha 10 kwenye ligi, hivyo kumfukuzia Fatuma mwenye mabao 20 na ambaye mchezo wa juzi kati ya timu yake ya JKT Queens dhidi ya Ruvuma Queens mambo yalikuwa magumu kwake na kutoka patupu huku Aisha Juma wa Alliance akiwa na mabao 13.

JKT Queens iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvuma Queens yaliyofungwa Zabela John na Mwamvua Seif huku Fatuma akicheza dakika 90 bila kuambulia bao baada ya mabeki wa wapinzani wao ‘kumficha’ na kushindwa kufurukuta.

Hata hivyo, alisema licha ya wapinzani wake kumfukuzia katika ufungaji bora, lakini hawamfikia kwani bado ana nafasi ya kufunga mabao mengi zaidi katika mechi zijazo.

“Ukweli mechi dhidi ya Ruvuma Queens ilikuwa ngumu kwani wapinzani wetu ni wazuri sana, ukiizungumzia timu bora kwenye ligi huwezi kuiacha Ruvuma Queens. Hata hivyo, siyo vibaya kutoka bila kufunga katika mchezo huo, kwani naamini nitafunga mabao mengi zaidi mechi zijazo,” alisema Fatuma ambaye kwa misimu miwili mfululizo alitwaa tuzo ya ufungaji bora.

Wachezaji wengine wanaoifukuzia tuzo ya ufungaji bora ni Aisha wa Alliance mwenye mabao 13, Hasnath Linus (Fountain Gate) aliyefunga tisa, Aisha Khamis (Yanga Princess) na Jamila Rajabu (Baobab Queens) waliofunga mabao manane kila mmoja.