Mo aongeza mzigo Simba

Mo aongeza mzigo Simba

SAA chache baada ya Tume ya ushindani wa kibiashara (FCC) kubainisha moja ya vitu ilivyohitaji kwenye mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ya Simba ni ufafanuzi juu ya kiasi halisi ambacho mwekezaji, Mohamed Dewji anatakiwa kuwekeza katika mabadiliko hayo ili kuondokana na mkanganyiko ulioko, imebainika kwamba mwekezaji huyo ameongeza mkwanja.

Juzi taarifa ya FCC ilibainisha sababu za mchakato huo kukwama ikiwa ni siku nne tangu Mo Dewji ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Simba kubainisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo kutoka kwa wanachama na kuwa kampuni umekwama kwenye tume hiyo.

Ingawa jana taarifa ya Simba ilieleza kwamba Mo Dewji alisema mchakato upo mikononi mwa FCC na si kwamba unakwamishwa au kucheleweshwa na tume hiyo kama ambavyo alieleza Jumapili kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya FCC kuijibu klabu hiyo juzi.

Taarifa ya FCC ilieleza kwamba pamoja na mambo kadha wa kadha ambayo hayakukamilika, tume ilitaka ufafanuzi wa kiasi halisi ambacho mwekezaji anatakiwa kuwekeza kwani kilichopo kwenye makubaliano ya awali ni tofauti na kinachotamkwa kwenye vyombo vya habari.

“Kiasi halisi ambacho mwekezaji, Bw. Mohamed Dewji anatakiwa kuwekeza ili kuondokana na mkanganyiko ulioko kati ya kiasi kilichotajwa kwenye Mkataba wa Makubaliano (Memorandum of Understanding) na kile kinachotajwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari,”ilisema taarifa ya FCC juzi.

Taarifa ya jana ya Simba iliweka wazi kiasi ambacho kipo kwenye makubaliano kuwa ni Sh 19.6 Bilioni.

“Hata hivyo mwekezaji ameamua atalipa zaidi ya kiwango kilichoainishwa kwenye makubaliano ili ifike bilioni 20,” ilieleza taarifa ya Simba jana. Hivyo kiasi kitakachoongezeka ni Sh400milioni.

Simba ilisema katika mchakato wa mabadiliko, kamati huru ya zabuni ilibainisha thamani ya asilimia 50 ya kampuni itakayoundwa kwa pamoja kati ya klabu na mwekezaji iwe Sh 20 Bilioni na Mo Dewji ndiye alionyesha nia na uwezo wa kulipa na kushinda zabuni hiyo.

“Baada ya Serikali kutoa maelekezo mapya mwekezaji apewe asilimia 49 na klabu asilimia 51, makubaliano yakawa kwamba mwekezaji anatoa Sh 19.6 Bilioni baada ya mchakato kukamilika na makubaliano yalikuwa mara baada ya mchakato kukamilika na Serikali kutoa idhini ndipo mwekezaji atatoa kiwango hicho cha fedha kilichobainishwa kwenye makubaliano,” ilieleza taarifa ya Simba.

Iliendelea kufafanua kwamba mchakato wa kutafuta idhini ulianzia Rita ambao walipaswa kuidhinisha kuhamisha mali na madeni kutoka kwa wadhamini kwenda kwenye kampuni na katika kufanikisha hilo walihitaji mihutasari ya uamuzi wa vikao vya wanachama

“Vilevile klabu ilishauriwa ipatikane idhini ya tume ya usindani wa biashara FCC, kwa maono ya FCC kwamba kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu ya Simba iliyosajiliwa Rita kwenda Simba Sports Club Company Limited taasisi ya kibiashara itakayosajiliwa Brela ni sawa na kampuni moja ya kibiashara kuungana na nyingine ya kibiashara

“Na kwamba kuna mashaka jambo hili linaweza kuathiri ushindani wa kibiashara, jambo ambalo tunaamini liko FCC kimakosa,” ilisisitiza taarifa ya Simba na kuongeza.

“Kwa kuwa tumeelekezwa kupitia FCC, kama klabu inayoheshimu mamlaka za Umma tulitii ili tukamilishe mahitaji yote yanayotakiwa haraka ili uwekezaji uanze na klabu yetu ijiendeshe kibiashara na kisasa zaidi.

Simba walifafanua kwamba walipeleka suala lao FCC Julai 23, 2020 kwa lengo la kutimiza masharti ya kukamilisha mchakato na iliendelea kuwa na mawasiliano chanya na FCC hadi oktoba 16, 2020 ilifanya kikao baina ya pande hizo mbili kwenye ofisi za Simba kwa lengo la kukamilisha mchakato.

“Siku chache baada ya kikao, klabu ilipokea barua yenye tarehe ya nyuma yaani Oktoba 13, 2020 inayowataarifu wadaawa wote wa mabadiliko ya uendesha wa klabu ya Simba juu ya uamuzi wa FCC kusitisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji ili kupitia masuala mbalimbali ya kisheria na kikanuni yaliyojitokeza wakati wa mchakato.

“Barua hiyo iliarifu kwamba FCC itawajulisha wadaawa kuanza tena kwa mchakato huo wa kupitia maombi ya klabu ya kubadili mfumo na siku tisa baadae, Oktoba 22, 2020 klabu ilipokea barua kutoka FCC ikiwataka kuwasilisha taarifa za ziada zinazohitajika kwenye kuidhinisha maombi ya klabu na kubadili mfumo wa uendeshaji,”.

Taarifa ya Simba ilisema Klabu iliomba kikao na FCC ili kufafanuliwa juu ya taarifa hizo mbili na kikao hakijafanyika na wanaendelea kufuatilia


WANASHERIA,WADAU WAFUNGUKA

Wakiichambua sintofahamu hiyo kati ya Tume na klabu ya Simba, baadhi ya wanasheria, wachumi, viongozi wa zamani wa soka na wadau mbalimbali walisema kuna walakini katika mchakato huo.

Mwanasheria wa kujitegemea, Kasanda Mitungo alisema; “Hoja za FCC ni kwamba Simba Sports Club Company Limited ni kama ilianza kufanya kazi wakati mchakato haujakamilika, uteuzi wa CEO kabla ya uwekezaji na mkanganyiko ulioko kati ya kiasi kilichotajwa kwenye mkataba wa makubaliano na kile kinachotajwa kwenye vyombo vya habari,”.

“Pia wanasema kuna vitu Simba hawajapeleka lakini hawajavisema, je ni nyaraka za kusapoti huo mchakato, nyaraka za malipo?, au ni baadhi ya taratibu hazikufuatwa?.

“Au ni mchakato haukuanza vizuri tangu mwanzo kuanzia kwenye klabu, kusajili brela, maombi ya notification hadi kulipia ada?,” alihoji Kasanda.

Alifafanua ada hiyo kuwa kwa kampuni ambayo thamani yake ni Sh 800 milioni hadi 25 Bilioni ada ni Sh 25 Milioni na kuanzia Sh 25 Bilioni hadi chini ya 100 Bilioni ada ni Sh 100 Milioni na kuanzia Sh 100 Bilioni kuendelea ada ni Sh 100 Milioni.

“FCC haijaweka wazi, hatuambiwi kitu gani hakijakamilika,” alisema ingawa Mdimi alipoulizwa jana sanjari na kiasi ambacho kipo kwenye makubaliano ya awali, aliomba aulizwe mkurugenzi kwa njia ya barua pepe na Mwanaspoti lilifanya hivyo lakini halikujibiwa.

Kasanda alifafanua kwamba kwa kuwa mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ya Simba bado haujakamilika, haikupaswa kujiendesha kisasa bali kujiendesha kwa mfumo wake zamani kwa kuwa na katibu mkuu na si CEO.

“Kifungu cha 60 cha sheria za ushindani kuna adhabu za jumla za kujiendesha bila taratibu, miongoni mwa adhabu zake ni kulipa faini ya asilimia tano hadi 10 ya thamani ya kampuni.

Mbali na Kasanda, wataalamu wa uchumi, Dickson Pastory ambaye ni mhadhiri mwandamizi wa chuo cha Biashara CBE, Dar es Salaam na profesa uchumi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Haji Semboja walisema katika mfumo huo kuna taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa hatua kwa hatua.

“Madeni ya klabu, mali za klabu, thamani ya klabu, ripoti ya ukaguzi na mambo mengine kadha wa kadha ni muhimu kwenye mchakato huo, hivyo uenda kuna ambavyo havijakamilika,” alisema Pastory.

Semboja alisema kwenye hilo “lazima sheria za nchi zifuatwe, sio kulipua lipua uenda ndicho kinakwamisha.”

Sintofahamu hiyo imewaibua pia wadau mbalimbali akiwamo aliyewahi kuwa mwenyekiti wa chama cha soka Tanzania (FAT) sasa TFF, Muhidin Ndolanga, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Simba Hamis Kilomoni na wenyeviti wa zamani wa klabu hiyo, Hassan Dalali na Swedi Mkwabi.

“Kwenye uwekezaji wa Simba kuna vitu vingi vimejificha, watu hawajaelezwa kipi ni kipi, binafsi naona tatizo linaanzia hapo,” alisema Ndolanga.

Kilomoni alisema; “Sikuwa mpinzani wakati ule, ila ninachosisitiza ni kwamba Simba ni timu ya wananchi.”

Swedi Mkwabi alisema hataki kuizungumzia klabu hiyo hivi sasa, lakini kama alivyowahi kusema wakati alipojiuzulu uenyekiti wa klabu hiyo muda ndiyo utazungumza.

Hassan Dalali alisema hajui kinachoendelea Simba, anachofahamu mchakato huo ulipitishwa basi, lakini umefikia wapi hafahamu.

______________________________________________________________

Na IMANI MAKONGORO