FCC yaibua utata mpya Simba

FCC yaibua utata mpya Simba

Muktasari:

  • FCC imeibua utata mpya baada ya kufafanua mambo kadhaa pamoja na kukanusha kuwa wao ndiyo kikwazo cha kuchelewa kwa mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ya Simba.

SIKU kadhaa baada ya Mwenyekiti ya Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji kueleza mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo bado upo kwa Tume ya Ushindani (FCC), tume hiyo imeibua utata mpya baada ya kufafanua mambo kadhaa pamoja na kukanusha kuwa wao ndiyo kikwazo cha kuchelewa kwa mabadiliko hayo.

Frank Mdimi, ambaye ni Ofisa Habari wa FCC, alilithibitishia Mwanaspoti kuwa taarifa iliyosambaa kwenye mitandao jana kuhusu Simba ni ya kweli na akibainisha kwamba kila kitu kuhusu kukwama kwa mchakato huo kimeelezwa ndani ya taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo, Tume ilieleza kufanya uchambuzi wa awali wa maombi ya Simba Sports Club Company Limited ya kupatiwa mwongozo wa kisheria chini ya Sheria ya Ushindani kuhusu namna ya kushughulikia mchakato wa mabadiliko unaohusisha kampuni za Simba Sports Club Holding Company Limited, Mo Simba Company Limited, Simba Sports Club Company Limited na Klabu ya Simba ya Aprili 24, 2019.

“Tume ilifanya vikao viwili baina yake na Simba Sports Club Company Limited hadi Julai 24, 2020 na wadaawa kuelewa mwongozo wa kisheria na kuahidi kuutekeleza kama walivyoelekezwa.

Taarifa hiyo ilieleza Oktoba 4, 2019, Tume ilitoa mwongozo wake kama ilivyoombwa na wadaawa kwa maandishi. Ambao walipaswa kwa mujibu wa sheria kujitathmini wenyewe na kupeleka maombi Tume kwa mujibu wa maelekezo ya kisheria.

“Katika ufuatiliaji Tume ilibaini viashiria kuwa Klabu ya Simba inaongozwa na Simba Sports Club Company Limited chini ya Mohamed Dewji kabla ya wadaawa hawajawasilisha maombi yao ya muungano (merger application) mbele ya Tume.

“Kitendo hiki, kwa mujibu wa mwenendo wa uchunguzi wa masuala ya ushindani ni kiashiria cha uvunjifu wa Kifungu cha 11 (2) cha Sheria ya ushindani, Januari 23, 2020, Tume ilianzisha uchunguzi wa jambo hili kwa mujibu wa sheria ya ushindani;

“Wakati uchunguzi unaendelea, Julai 23 2020, Tume ilipokea maombi ya muungano wa makampuni (merger application) kutoka kwa wadaawa, wakiijulisha Tume nia yao ya kuichukua Klabu ya Simba na kuiendesha kama kampuni chini ya kampuni mpya waliyoianzisha ya Simba Sports Club Company Limited.

“Tume iliyafanyia uchambuzi wa awali maombi hayo na Julai 30,2020, iliwajulisha wadaawa kwamba taarifa walizoziwasilisha mbele ya Tume hazikukidhi matakwa ya sheria ya ushindani na hivyo kuwataka wawasilishe taarifa husika ili mchakato wa uchambuzi uendelee;

“Oktoba 13, 2020, Tume ilisitisha kwa muda mchakato wa uchambuzi wa maombi ya muungano wa kampuni na kuwajulisha wadaawa ikilenga kupata taarifa na ufafanuzi zaidi kutoka kwa wadaawa na wadau wengine.”

FCC ilisema ilitaka ufafanuzi kuhusu uteuzi wa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Klabu ya Simba kabla ya uwekezaji kufanyika, kiasi halisi ambacho mwekezaji, Dewji anatakiwa kuwekeza ili kuondokana na mkanganyiko ulioko kati ya kiasi kilichotajwa kwenye mkataba wa makubaliano na kile kinachotajwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

“Hadi Novemba 18, 2020, uongozi wa Klabu ya Simba haukuwa umekamilisha taarifa, nyaraka pamoja na ufafanuzi wa masuala hayo na mengine kadha wa kadha.

“Ucheleweshwaji wa mchakato wa kubadili mfumo wa uendeshaji wa Klabu ya Simba unatokana na mwitikio hafifu wa kampuni ya Simba Sports Club Company Limited wa kuwasilisha taarifa kamilifu na kwa wakati mbele ya Tume katika kufanikisha uchunguzi tajwa hapo juu na Tume haihusiki na ucheleweshwaji wa mchakato kama ilivyoelezwa na viongozi wa Timu ya Simba,” ilisema taarifa hiyo.

Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda na vigogo wengine wa klabu hiyo jana hawakuwa tayari kufafanua yaliyomo kwenye taarifa hiyo licha ya kupigiwa simu zao bila majibu.

_______________________________________________________________

Na IMANI MAKONGORO